Habari za Punde

Balozi Corner: Utawala wa Malkia Elizabeth umeleta maendeleo


Na Salum Vuai, MAELEZO

KIPINDI cha miaka 60 tangu Malkia Elizabeth II, akalie kiti nchini Uingereza maendeleo makubwa yameshuhudiwa katika nchi za Jumuiya ya Madola ambazo zilikuwa makoloni ya taifa hilo ikiwemo Zanzibar.

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Diane Corner, alisema hayo wakati akihutubia kwenye hafla ya kuadhimisha siku maalumu ya Malkia kutimiza umri huo madarakani, iliyopewa jina la 'Diamond Jubilee, ambayo ilifanyika juzi usiku kwenye ofisi ndogo ya ubalozi huo Migombani, Zanzibar.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Juma Shamuhuna, sambamba na kuhudhuriwa na mabalozi wadogo mbalimbali waliopo Zanzibar.

Miongoni mwa mafanikio hayo, alisema Balozi Corner, ni kukombolewa kwa makoloni hayo, kukua kwa demokrasia katika nchi hizo, pamoja na kuimarika utawala bora.

Corner alisifia umoja na mshikamano kati ya nchi zinazounda Jumuiya ya Madola, akisema zinafanya kazi kubwa kuhakikisha demokrasia katika nchi zao inakuwa imara kuliko ilivyokuwa kabla.

Aidha alieleza kuwa, nchi za jumuiya hiyo zimeweza kusimamia chaguzi 85 katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ukiwemo ule wa Tanzania mwaka 2010, huku akisema jumuiya imedhihirisha ukomavu wake kwa kuruhusu demokrasi ikuwe kwa namna nchi hizo zinavyopenda.

Alitoa mfano wa Zanzibar, ambapo wananchi wake walifanya uamuzi wa kidemokrasia mwaka 2010, kwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi wa 2010, na kuzika siasa za mfarakano, uhasama na chuki.

Alifahamisha kuwa, Umoja wa Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola, (CPA) unawakutanisha wajumbe wa nchi hizo katika kujadili wajibu wao, kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka miongoni mwao juu ya mambo ya msingi hasa mtandao wa majaji wakuu, bodi za kitaaluma na mfungamano wa michezo, na kusema anajua kwamba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wamekuwa na mchango mkubwa katika CPA.

Kuhusu uchumi wa nchi hizo, Balozi Corner alisema nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola ni miongoni mwa zile ambazo uchumi wao unakua kwa haraka duniani, akisema mapato ya mataifa hayo yameongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Aliongeza kuwa idadi ya watu wa tabaka la kati katika nchi hizo, imezidi kwa karibu bilioni moja ndani ya kipindi hicho ambapo imefikia asilimia 31 ya watu wote duniani.

Aidha, alieleza kuwa nchi nyingi wanachama wa jumuiya hiyo, zina mahusiano ya muda mrefu katika biashara, na kutoa mfano wa Tanzania ambako Uingereza inabaki kuwa muwekezaji mkubwa na kwamba uwekezaji wake unazidi kuimarika ukiwa umepiga hatua kwenye ukanda wa gesi katika bahari ya ukanda wa kusini.

Hata hivyo, alisema kuwa, maendeleo hayo hayakupatikana kirahisi hasa ikizingatiwa kuwa katika mwaka 1952 wakati Malkia Elizabeth wa II akianza kukalia kiti hicho, dunia ilikuwa tafauti ikiwa ndio kwanza imetoka katika vita vya kutisha vya dunia, na kugawanyika kwa mitazamo ya kiitikadi na tafauti za ukomunisti, usoshalisti na ubepari.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna, alimpongeza Malkia kwa jitihada zake kubwa kuhakikisha Jumuiya ya Madola inakua imara, ambapo sasa ina nchi wanachama 54.

Alisema, katika kipindi cha uongozi wa Malkia Elizabeth, kumeshuhudiwa uhusiano kati ya Zanzibar na Uingereza ukiimarika maradufu, chini ya msingi madhubuti wa demokrasi, utawala bora na wa sheria, pamoja na haki za binadamu.

Aidha, Shamuhuna alisema Zanzibar ilipata baraka za ziara ya mwana wa Malkia Prince Charles na mkewe Camilla, waliyoifanya mwezi Novemba mwaka 2011, ambapo alieleza kuwa, Wazanzibari walivutiwa sana na ujio huo adhimu wa kihistoria.

Pamoja na kumpongeza Malkia kwa uongozi wake bora tangu akalie kiti hicho mwaka 1952, Waziri Shamuhuna, alitoa shukurani kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar na wananchi wake, na kumtakia kiongozi huyo na nchi yake mafanikio zaidi na umri mrefu.

Ifikapo Juni 5, mwaka huu, Malkia Elizabeth wa II atatimiza miaka 60 tangu atawazwe kushika nafasi hiyo, ambapo ofisi za balozi za Uingereza duniani kote ziko katika wiki za maadhimisho hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.