Habari za Punde

Matarumbeta Nursery Inahitaji Msaada Wako

 Hii ndiyo skuli ya Maandalizi ya Matarumbeta iliopo Wilaya ya Mjini Unguja ambayo ina Madarasa matatu ikisimamiwa na uongozi wa mtaa. Ina wanafunzi mia moja. Wazazi hutakiwa kulipia ada kila mwezi kwa mtoto shilingi elfu tatu.

 Hawa ni baadhi ya wanafunzi wa Skuli hii iliopo Mwembe Matarumbeta wakiwa katika nyuso za furaha baada ya kutembelewa na blog ya Zanzinews ili kujionea maendeleo pamoja na changamoto zinazowakabili

Hili ni moja ya darasa skulini hapo ambapo watoto wanakaa chini kwenye mabusati badala ya kuwa na vikalio, jengo linalotumika kusomeshea kuta zake zinahitajia rangi na katika kipindi cha masika na mvua huwa na wakati mgumu kwani sehemu kubwa ya paa inavujisha. Sakafu yote takriban imeshatiwa viraka na iko hoi bin taaban.


Hapa watoto wakiwa katika mapumziko na skuli hii ingawa ina wanafunzi mia moja ila wana choo kimoja tu na hawana vifaa vya kuchezea watoto hasa wa skuli za maandalizi kama Nursery, Toys zinazofundishia, wanahitajia pia vifaa vya kufundishia kama Manila, rangi kadi za aina mbali mbali kama za Nambari au Silabi ( A,BC).

Walimu tayari wameshajitolea muda wao na si Waajiriwa wa Serikali ambao hulipwa mshahara hawa ni wa kujitolea na zaidi hutegemea ada za wanafunzi ambazo hazilipwi kwa wakati na pengine kutolipwa kabisa. Maendeleo ya wanafunzi yanatia moyo ila hawana vifaa vya kuwasaidia kuweza kutekeleza wajibu wao kisawasawa.

Wanachomba kwenu yeyote atakaebahatika kusoma habari hizi kama anaweza kusaidia kutatua changamoto wanazokabiliana nazo na  walizoorodhesha wanakaribishwa. Kama kuwaletea vifaa vya kusomeshea au mwengine kuchangia mabati, mwengine kukarabati sakafu na kadhalika.

Kama uko tayari kutoa msaada wa aina yoyote tuandikie kupitia othmanmaulid@gmail.com au Wasiliana na Mwalimu Mkuu 0778311704

1 comment:

  1. Majibu ni rahisi hapa, ni kuhamasisha wazazi kutoa kipao mbele kwa elimu ya watoto wao.

    Badala ya kushughulikia mambo yasiyo na maana kama vile ushongo na kuongeza wake kiholela, ipo haja sasa tukatenga kidogo tukipatacho kusaidia elimu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.