TAMKO LA SHIRIKA LA KAZI DUNIANI KANDA YA AFRIKA MASHARIKI NA RWANDA
ILIYOTOLEWA NA BI FATMA M. RASHID KWA NIABA YA
MKURUGENZI WA SHIRIKA LA KAZI DUNIANI
KANDA YA AFRIKA MASHARIKI NA RWANDA
BW. ALEXIO MUSINDO MEI DAY, 2012
BWAWANI HOTEL.
Leo, Shirika la Kazi Duniani
linaungana na Serikali, waajiri na wafanyakazi na vyama vyao, kusherehekea Siku
ya Wafanyakazi Duniani. Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani
Kanda ya Afrika Mashariki na Rwanda, bw. Alexio Musindo ninayo heshima kuwaletea
salamu za Shirika kwa ajili ya siku hii muhimu – siku ya kutafakari kuhusu haki
za msingi mahala pa kazi na majadiliano ya kijamii ambayo yanalenga kuhusu
uhuru na utu wa binadamu; pia kama zana za kuzidisha uzalishaji na maendeleo
linganifu.
Wafanyakazi ni kitovu cha ustawi wa
Jamii. Wafanyakazi ni kichocheo muhimu cha mikakati ya maendeleo na nafasi yao inahitaji kutambuliwa
katika maeneo kama ujira, mazingira na masharti ya kazi. Hii husaidia sana
katika kuhimiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuwaimarisha wafanyakazi
wenyewe, familia zao na jamii kiujumla.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi
Duniani Ndugu. Juan Somavia katika salamu zake za Siku ya Mei Mosi mwaka huu
ameeleza kuwa, “…Kufanya kazi kinadhifu na kwa bidii ndio chanzo cha heshima
kwa binadamu, uimarishaji wa familia, kuleta amani katika jamii na pia ni
chanzo cha kuaminika kwa uongozi wa kidemokrasia…Katika maeneo mengi
ulimwenguni tumepoteza mtazamo wa msingi kuwa kazi sio bidhaa”.
Mgogoro
wa kiuchumi na kifedha duniani umeathiri kwa haraka sana uchumi halisi duniani
na kuzidisha tatizo la ukosefu wa ajira kwa kuwaacha watu zaidi ya milioni 200 bila ajira duniani,
ikiwa ni pamoja na karibu vijana milioni 80, wengi wakiwa wanaishi kwa kiasi
cha Dola za Kimarekani 1.25 tu kwa siku.
Kama mchango wa kushughulikia
changamoto hizi, Shirika la Kazi Duniani limeuteua ‘ Mwezi Machi 2012’,
kama ‘Mwezi wa Ajira kwa Vijana’ na
limeamua kuwa mada ya “Tatizo la Ajira
kwa Vijana” kuwa moja ya ajenda kuu za Kikao cha 101 cha Mkutano Mkuu wa mwaka
wa Shirika la Kazi Duniani mnamo Juni mwaka huu huko Geneva.
Kwa malengo hayohayo, mkutano wa
kitaifa unaohusu ajira kwa vijana uliitishwa jijini Dar es Salaam hivi karibuni
ili kujadili ajenda ya ajira za staha kwa vijana nchini na
kubadilishana mawazo kuhusu yale mazuri yaliyokwishafanyika. Zanzibar nayo
ilishiriki katika mkutano huo. Katika mkutano huo tumeshuhudia juhudi mbalimbali zilizokwishachukuliwa kujumuisha masuala
ya ajira katika mikakati ya maendeleo ya kitaifa, yaani (MKUKUTA) na (MKUZA).
Ili kusonga mbele, Shirika la Kazi
Duniani linaonelea kuwa ulimwengu unahitaji kubadili muundo wa sasa wa ukuaji
kiuchumi duniani kwani muundo uliopo
umejenga ukwasi mkubwa ulioenea katika mikono michache. Muundo huu umeshindwa
kuandaa aina ya ukuaji jumuishi tuliotegemea.
Shirika linapendekeza aina nyingine
ya ukuaji kiuchumi ambao unajali mazingira na kulenga mahitaji ya watu,
yaani muundo ambao lengo lake kuu ni
kuongeza ustawi wa watu hivyo kupima mafanikio kutokana na idadi ya ajira na
sio asilimia ya ukuaji wa jumla wa Pato la Taifa (GDP).
Hivyo tunahitaji kuchukua hatua
kadhaa kuhakikisha kuwa tunaelekea katika enzi mpya ya haki ya kijamii (new era
of social justice) kama namna ya kusonga mbele katika kushughulikia baadhi ya
masuala niliyokwisha yaeleza kabla na baadhi yake ni:
·
Kuhakikisha kuwa malengo ya kuandaa nafasi za ajira
yanakuwa kipengele muhimu cha sera ya uchumi mpana (Microeconomic policy)
pamoja na kupunguza mfumuko wa bei, pia kuchochea uwekezaji na kuhimiza
uwekezaji katika biashara ndogondogo, sekta zinazotoa nafasi nyingi za ajira,
masoko jumuishi ya ajira na ukuzaji wa ujuzi wa aina mbalimbali.
·
Kutambua kuwa haki za msingi kazini na majadiliano ya
kijamii ambayo ni sehemu ya uhuru na heshima ya kibinadamu pia ni kama zana ya
kuzidisha uzalishaji, tija na maendeleo linganifu.
Ili haya yafanikiwe na kulenga
kwenye kuwa na kazi zenye staha, ni muhimu kuimarisha suala la majadiliano ya
kijamii na lile la utatu. Shirika la Kazi Duniani limeendelea kufanya kazi na
asasi mbalimbali za masuala ya kazi kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita kupitia
mradi wake wa kuboresha uelewa na matumizi ya sheria za kazi ili kuongeza
ufahamu kati ya waajiri na wafanyakazi kuhusu wajibu na haki zao za msingi
kazini, kwa kuzingatia sheria za kazi nchini. Kazi iliyofanyika imepelekea
kuongezeka kwa uwajibikaji katika mifumo ya uongozi kazini hasa katika
utekelezaji wa sheria za kazi. Yafuatayo ni baadhi tu ya mafanikio:
·
Kusaidia kuchapishwa kwa vipeperushi vinavyohusu kitengo
cha usuluhishi wa migogoro ya kazi
·
Kusaidia mafunzo ya darasani na kivitendo kwa wakaguzi kazi
pamoja na kuifanyia majaribio tool, checklist iliyotengenezwa kutokana na
mafunzo yaliyopita nyuma.
·
Kutoa mafunzo kwa maafisa kazi na bodi ya kazi ya ushauri
juu ya sheria za kazi, mijadala ya pamoja, utatu na mikataba ya shirika la kazi
duniani.
·
Mafunzo ya usuluhishi wa migogoro ya kazi kwa kitengo cha
usuluhishi wa migogoro.
·
Kuanzishwa kwa database ya masjala ya kitengo cha
usuluhishi wa migogoro ya kazi.
·
Kusaidia kitengo cha usuluhishi wa migogoro kuunganishwa na
kitengo cha usuluhishi migogoro ya kazi cha huko bara na kupata mafunzo
kivitendo kwa wiki mbili.
·
Kitengo cha usuluhishi wa migogoro na mahakama ya kazi
kupatiwa vifaa vya ofisi kama komputa na saver kwa ajili ya kurahisinsha
utekelezaji wa kazi za kila siku.
·
Kusaidia kuanzishwa kwa kitengo cha usuluhishi wa migogoro
ya kikazi.
·
Kusaidia mahakama ya kazi kuhifadhi maamuzi ya kesi za kazi
kwa njia ya kompyuta.
·
Kusaidia mkutano wa utatu wa viongozi na wadau wetu ambao unakutanisha
viongozi wa Wizara ya Kazi, Jumuiya ya Waajiri na Wafanyakazi wa Zanzibar na wa
Tanzania bara kuzungumzia juu ya masuala ya kazi.
Ni matumaini yetu makubwa kuwa
shughuli hizi zitachangia katika kuimarisha majadiliano ya kijamii na kuboresha
uhusiano na ushirikiano mahala pa kazi.
Kama wengi tunavyofahamu tayari,
viwango vipya vya kazi vya kimataifa kwa moja ya vikundi vya wafanyakazi
vilivyo katika mazingira hatarishi kwenye uchumi usio rasmi yaani – “kazi zenye
staha kwa wafanyakazi wa ndani” vilipitishwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirika
la Kazi Duniani wa 100, yaani Mkataba Na. 189, na pendekezo Na. 201 (2011).
Napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Tanzania hasa Zanzibar na
washirika wetu ambao ni jumuiya ya wafanyakazi na waajiri kwa juhudi zao
walizofanya kuhakikisha viwango hivyo vinapitishwa na kwa juhudi ambazo tayari
zinaendelea kufanyika kama maandalizi ya kuridhia mkataba huo.
Kwa
mara nyingine, napenda kukuhakikishia ndugu mgeni rasmi nia na utayari wa Umoja wa Mataifa kwa ujumla,
kupitia Mpango wake wa Msaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDAP), na
Shirika la Kazi Duniani kusaidia shughuli zinazolenga kuimarisha majadiliano ya
kijamii miongoni mwa wadau wote kama njia ya kukuza kazi zenye staha kwa wote.
Ahsanteni
Sana!
No comments:
Post a Comment