Habari za Punde

Wafanyakazi wavamia bodi ya korosho

Na Fatuma Kitima, DAR ES SALAAM
WAFANYAKAZI wa viwanda vya kubangua korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na Pwani, wamevamia ofisi za Bodi ya korosho Tanzania kudai mapunjo ya mishahara yao.

Wafanyakazi hao walisema kuwa bodi hiyo imekuwa ikiwazungusha kwa muda mrefu kwa kutowalipa mapunjo hayo tangu walipowaachisha kazi miaka 20 iliyopita.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, walisema wamefikia hatua ya kufika kwenye ofisi za bodi hiyo baada ya bodi hiyo kutoonesha nia ya kuwalipa na wakati mwingine ikitoa kauli za kuwakashifu.

Inakisiwa kuwa wafanyakazi zaidi ya 2,500 wanadai mapunjo ya mishahara yao, katika kazi hiyo kila mwezi Desemba walikuwa wanapewa likizo, mwaka 1992 waliambiwa kuwa warudi nyumbani mpaka watakapoitwa tena kutokana na kutokuwepo kwa malighafi na hivyo walipewa fedha kidogo.

Mmoja kati ya wafanyakazi hao, Stumai Mohamed alisema kuwa baada hapo hawakurudishwa kazini na wala hawakupewa barua za kuwasimamisha kazi licha ya kwamba walikuwa ni waajiriwa.

Alisema kutokana na kuwepo udanganyifu baada ya likizo hiyo wameifikisha bodi hiyo mahakamani ambapo mara nyingi wamekuwa wakishinda, lakini hawalipwi mapunjo hayo na hivyo kuwazidishia usumbufu mkubwa.

Alisema katika Bunge la Bajeti mwaka jana suala lao lilizungumzwa, na waandishi waliandika kuwa watalipwa malipo yao.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Bodi hiyo, Ugumba Kilasa aliwataka wafanyakazi hao kumwambia mwanasheria wao apeleke nakala ya hukumu kama wanavyodai kuwa walishinda kesi ili bodi iwalipe.

Awali akizungumza na waandishi Kilasa alisema wafanyakazi hao tayari walishalipwa mapunjo yote wanayodai na hivyo anashangaa hatua ya kuibua madai ya kutaka kulipwa tena.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.