Na
Hafsa Golo
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheri,
amesema sera mpya ya Utawala Bora ni miongoni mwa mchakato utakaohakikisha
shughuli za serikali zinafuata misingi ya katiba, utawala wa sheria na
kuimarisha maadili.
Waziri
huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani mjini hapa, kwenye
hafla fupi ya uzinduzi wa sera ya utawala bora, ambayo ilihudhuriwa na
watendaji wa ngazi mbali mbali serikalini na asasi za kiraia.
Waziri
huyo alisema moja ya faida ya kuwepo kwa sera hiyo ni kutoa muongozo juu ya
mgawanyo wa madaraka katika utekelezaji wa majukumu ya serikali, kufuatwa kwa
maadili pamoja na utamaduni wa utayarishwaji wa watendaji na viongozi wa
kuchaguliwa.
Alisema
awali misingi ya utawala bora ilikuwa haijumuishwi katika sera za kitaifa,
hivyo kuzinduliwa kwa sera hiyo ni miongoni mwa mikakati ya kuifuata misingi
hiyo kivitendo.
Alifahamisha
kuwa miongoni mwa malengo ya kuwepo sera hiyo kutaisaidia jamii kutekeleza
majukumu kwa kufuata misingi ya utawala bora, hali itakayosukuma mipango ya
kufikiwa kwa maendeleo.
"Wizara
yangu itahakikisha inafuatilia tathmini ya utekelezaji wa sera hiyo, na kutoa
taarifa kila mwaka ya utawala bora, taarifa hiyo itakuwa ya wazi na itaonesha
maeneo yaliyofanya vizuri pamoja na kuonesha changamoto zilizopo ili tuweze
kutafuta njia za kuzishughulikia changamoto hizo", alisema.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo Joseph Meza, alisema kuwa itaimarishwa
mikakati ya utekelezaji wa sera hiyo na kwamba misingi ya sheria zilizowekwa
nchini inafuatwa.
Meza
alisema sera hiyo mpya itakuwa dira na chombo muhimu cha kufanyia tathmini na
kutoa muelekezo juu ya namna utawala bora unavyotekelezwa nchini.
Alisema
wakati wa utayarishwaji wa sera hiyo, juhudi zilichukuliwa katika
kuwashirikisha wadau ili kuhakikisha michango yao inapatikana, ambapo michango
hiyo ilikuwa chachu ya kukamilika kwa sera hiyo.
Katibu
huyo alisema imerahisishwa kila madau kuisoma sera hiyo kwani imeandaliwa kwa
lugha za kiingereza na Kiswahili pamoja na kuwepo kwa nukta nundu ambazo
zinawawezesha watu wasioona kuweza kuisoma.
Kwa
upande wa Mwakilishi wa watu wasioona Fatma Djaa Chesa, aliiomba serikali kutoa
elimu kwa wizara husika ili iweze kuzingatia umuhimu wao wa kuelewa mambo
muhimu yanafanyika katika serikali yao kwa kuwachapishia maandishi ya nukta
nundu na kuwafikishia sehemu walipo.
No comments:
Post a Comment