Na Tatu Khamis
JAMII nchini imetakiwa kuwathamini watu wenye ulemavu, iwache vitendo vya udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu kwa lengo la kuleta usawa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Watu wenye Ulemavu wilaya ya Kaskazini ‘B’, Haji Khamis Nyange, alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Mahonda.
Alisema watu wenye ulemavu wanahaki ya kuishi na kupatiwa haki sawa na kushirikishwa juu ya mambo mbali mbali yanayohusu jamii lakini wamekuwa wakitengwa na kutopewa ushirikiano jambo ambalo limekuwa likiwavunja moyo.
Alisema kufanya hivyo ni kuwanyima fursa na haki zinazotolewa na vitengo vilivyo jibebesha dhima hiyo ya kuwatumikia watu wenye ulemavu.
Alifahamisha baadhi ya vitendo wanavyofanyiwa watu wenye ulemavu si vizuri ambavyo huwakosesha hamu ya kushiriki katika mambo mbali mbali ya kijamii na hata ya kitaifa kwa ujumla.
Aidha alisema huduma za kijamii zinapaswa kupewa watu wote na wala sheria haijawatenganisha nani wa kupatiwa haki sawa, lakini jamii bado haijaelewa na hivyo baadhi ya wazazi huwafungia ndani watoto wao wenye ulemavu kwa sababu tu ya kutoelewa watu wenye ulemavu wana nafasi gani katika jamii.
Nae Katibu wa Umoja wa Watu wenye Ulemavu, Hababuu Mohammed Abdallah alisema mtu mwenye ulemavu ana haki ya kupatiwa huduma za afya mbali mbali na kuchukuliwa hatuwa za kumkinga na jambo linaloweza kumpa ulemavu zaidi.
No comments:
Post a Comment