Habari za Punde

TALGWU Yapinga Ongezeko la Asilimia 20

Na Fatuma Kitima, DAR ES SALAAM 

CHAMA cha Wafanyakazi wa serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), kimesema hakijaridhishwa na kiwango cha ongezeko la asilimia 20 ya kima cha chini cha mishahara kwa mwaka 2012/2013.

 Katibu Mkuu wa chama hicho Sudi Madega alisema kima cha chini kilichopendekezwa na chama hicho ni shilingi 315,000, ambacho kingewawezesha wafanyakazi kupata unafuu wa maisha. 

 Alisema kutokana na ongezeko hilo la asilimia 20 litapelekea kima cha chini cha mshahara ambacho ni shilingi 150,000 kufikia shilingi 170,000 ongezeko ambalo ni dogo ukilinganisha na kupanda kwa gharama za maisha. 


 Akizungumza Dar es Salaam jana, Madega alisema kitendo cha serikali kuongeza kiwango hicho ni cha kikatili kutokana na kutokidhi mahitaji ya wafanyakazi kwa ujumla. Madega alichanganua kuwa, licha ya mishahara midogo wanayolipwa wafanyakazi hao katika sekta mbalimbali, lakini bado serikali imeshindwa kulipa madeni yao kwa wakati na kuwafanya waendelee kuishi maisha magumu. 

 Alifafanua kuwa mfumko wa bei umeongezeka kutoka asilimia 10.9 kwa mwaka jana hadi kufika asilimia 18 kwa mwaka huu, jambo linalohatarisha maisha ya wafanyakazi na kuwafanya waishi maisha magumu zaidi. 

Alisema kukosekana kwa kiwango kilichopendekezwa kitasababisha kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara baina ya waajiri na wafanyakazi katika sehemu za kazi. “Serikali inatakiwa kuwa makini katika kufanya uchunguzi wa watendaji wa serikali za mitaa wanaotuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma,ikiwemo kuwachukulia hatua za sheria badala ya kuwachanganya na wale wasiohusika", alisema Madega. 

 Katibu huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Ofisi ya waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kutekeleza ahadi ya kutoa mafunzo kwa madiwani 4,451, jambo ambalo litapunguza migongano kati yao na wakurugenzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.