Habari za Punde

Maalim Seif: Tunathamini misaada jumuiya ya kimataifa


Na Hassan Hamad, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, amesema jamii ya kimataifa imekuwa nguzo muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar kutokana na mchango wake kwenye sekta mbali mbali ikiwemo ya afya.

Maalim Seif alieleza hayo huko nyumbani kwake Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar alipofanya mazungumzo na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Dk. Ad Koekkoek.

Alisema kutokana na mchango wa jumuiya hiyo, kwa kiasi kikubwa umekuwa ukisaidia serikali kufikia malengo iliyojiwekea ikiwa pamoja na kuifanya hospitali ya Mnazimmoja kuwa ya rufaa.


Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imekuwa ikithamini misaada hiyo kwani inasaidia kutimiza malengo ya kimaendeleo kwa wananchi, na kuiomba nchi hiyo kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo baina yake na Zanzibar.

Aidha Maalim Seif, alisema serikali itaendelea kuitunza hazina ya amani iliyopo nchini, na kwamba haitomvumilia mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuivuruga amani iliyopo.

Alisema  amani ni kitu muhimu na adhimu katika kukuza uchumi wa nchi, hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar inategemea zaidi sekta ya utalii ambacho ni miongoni mwa chanzo kikuu cha mapato yake ya fedha za kigeni.

Maalim alisema nia ya serikali ni kuendeleza utalii wa kimazingira katika kisiwa cha Pemba ni kuwawezesha wananchi wa kisiwa hicho kuweza kushiriki moja kwa moja katika shughuli za utalii, ili kuweza kuongeza kipato chao hali itakayowawezesha kupunguza ukali wa maisha.

Alisema serikali ina nia ya kujenga bandari mpya ya kibiashara katika eneo la mpigaduri ambayo itaziwezesha meli kubwa za nje kuweza kufunga gati na kurahisisha shughuli za kibiashara katika mwambao wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Dk. Ad Koekkoek, alisema katika kukuza sekta ya utalii, ni vyema kwa serikali kuandaa utaratibu wa kuyashawishi mashirika mengi zaidi ya ndege kufanya safari zake moja kwa moja hadi Zanzibar.

Alisema hatua hiyo itarahisisha shughuli za kitalii na kuongeza idadi ya watalii kila mwaka, na hatimaye kukuza uchumi wa taifa na pato la wananchi.

Nae mkuu wa masuala ya uchumi na biashara kutoka ubalozi huo, Dirk-Jan Brouwer, alisema Uholanzi itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha huduma za wananchi hasa kwenye sekta ya afya, ambapo kwa sasa wamekuwa wakisaidia upatikanaji wa vifaa mbali mbali vya matibabu katika hospitali ya Mnazimmoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.