Habari za Punde

Maazimio ya Baraza Kuu CUF


MAAZIMIO YA KIKAO CHA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA KILICHOFANYIKA UKUMBI WA SHABAN HAMISS MLOO MJINI DAR ES SALAAM TAREHE 14-15 Julai, 2012.

Yametangazwa leo tarehe 17/07/2012,Ofisi za CUF Buguruni mbele ya waandishi wa habari.

Baraza Kuu la Uongozi Taifa la The Civic United Front (CUF- Chama Cha Wananchi) limekutana katika kikao chake cha kawaida kwa mujibu wa Katiba ya Chama, kikao ambacho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mhe. Prof Ibrahim Lipumba na kufanyika katika Ukumbi wa Shabani Hamisi Mloo , Dar es salaam, Tarehe 14-15 Julai, 2012. 

Katika kikao hicho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limepokea, limejadili na kuzifanyia maamuzi Agenda mbalimbali zilizowasilishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ikiwa ni pamoja na;
1. 1. Utekelezaji wa Kazi za Chama kipindi cha Oktoba 2011-juni 2012
2. 2. Maandalizi ya Uchaguzi mdogo Jimbo la Bububu
3. 3. Msimamo wa Chama katika mchakato wa Maoni ya Wananchi kuhusu uandikaji wa Katiba mpya ya Tanzania.
4. Uimarishaji wa Chama kupitia Jumuiya ya Vijana.
5. Hali ya Kisiasa Nchini.
Baada ya Mjadala wa kina kuhusiana na agenda hizo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:

Utekelezaji wa Kazi za Chama kipindi cha Oktoba 2011-juni 2012

1. Baraza Kuu limepokea Taarifa ya Kazi za Chama kwa kipindi cha Oktoba 2011 hadi 2012. Baraza limeipongeza Kamati ya Utendaji kwa Kazi ilizofanya na kusimamia kwa kipindi pamoja na changamoto za kiutendaji zinazowakabili. Baraza Kuu limetoa msisitizo kwa Chama kuendelea kujipanga .
Kuhusu Maandalizi ya Uchaguzi Bububu
1. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeridhia lengo la Chama kushiriki katika Uchaguzi wa marudio katika Jimbo la Bububu na kuhakikisha chama kinashinda kwa sababu jimbo hilo ni ngome kubwa ya CHAMA na hasa baada ya kutathmini matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Kuhusu uimarishaji wa Chama kupitia Jumuiya ya Vijana
1. Baada ya kazi kubwa iliyofanywa na jumuiya za chama na kuonekana kuwa zinapaswa kuimarishwa zaidi, hususani jumuiya ya vijana taifa (JUVICUF), Baraza Kuu limejadili na kukubaliana kufanya mabadiliko katika nafasi mbali mbali za Uongozi ndani ya Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kubadilisha baadhi ya wajumbe waliokuwepo awali. Viongozi walioteuliwa na kuthibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ni hawa wafuatao:-

S/N JINA NAFASI
1 Katani A.Katani M/kiti
2 Yusuph K. Makame M/Mwenyekiti
3 Khalifa A. Ali Katibu
4 Thomas D.C. Malima Naibu Katibu
5 Sonia Magongo Mjumbe
6 Bonifasia Mapunda Mjumbe
7 Kuruthumu Mchuchuli Mjumbe
8 Said Maulid Mjumbe
9 Ashura Mustapha Mjumbe
10 Hamidu Bobali Mjumbe
11 Ahmed Mudhihir Mjumbe
12 Shomvi R Issa Mjumbe
13 Faustin Khalfan Mjumbe
14 Suleiman S. Abdallah Mjumbe
15 Biubwa M. Mselem Mjumbe
14 Pavu J. Abdallah Mjumbe
15 Gora J. Hamis Mjumbe
16 Hafidh A. Hafidh Mjumbe
17 Ayoub Y. Khamis Mjumbe

Kuhusu mgomo wa madaktari nchini;

1. Baraza kuu limesikitishwa na mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini kwa zaidi ya miezi saba sasa bila Serikali ya CCM kuwa na mkakati wenye malengo ya kuondoa tatizo lililopo. Kuendelea kwa mgomo huo kumesababisha kusuasua kwa huduma za Afya kunakowasababishia mateso makubwa wananchi wa tabaka la hali ya chini na wengine kufa kwa kukosa tiba katika kipindi muafaka.

2. Baraza Kuu linawasihi Madaktari wote warejee kazini ili kuokoa maisha ya Watanzania wenzao wasio na uwezo wa kwenda kutibiwa hospitali zinazotoa pesa nyingi, sambamba na hilo tunaiomba Serikali iwaombe Madaktari wote waliosaini kuacha kazi warejee kazini.

3. Kuendelea kuwafukuza na kuwatishia si kutatua tatizo hili kwa sababu limekuwepo muda mrefu na madaktari wana madai ya msingi ya kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wananchi pamoja na mishahara yao, madai haya yasidharauliwe kwa sababu yana mantiki kubwa japokuwa hayapaswi kutumiwa kupoteza roho za watu kwenye mgomo. Tunaitaka Serikali ya CCM ihakikishe inatekeleza madai yote ya msingi yanayolalamikiwa na Madaktari, pia kuhakikisha inaboresha zaidi huduma za Afya.

4. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limelaani kitendo cha kutekwa, kuteswa na kuhujumiwa kwa kiongozi wa madaktari ndugu. Ulimboka , Baraza Kuu linaitaka serikali iunde tume huru ya wataalam na isiyohusisha usalama wa taifa wala Jeshi la polisi ili suala hili lichunguzwe na matokeo ya uchunguzi yawekwe hadharani.

5. Mgomo wa madaktari umechukua nafasi kubwa katika vyombo vya habari haidhuru ni sehemu ndogo ya huduma za afya. Watanzania wachache sana wanaopata fursa ya kuonana na daktari. Wengi wanategemea huduma za zahanati na vituo vya afya ambavyo vina hali mbaya sana. Hakuna huduma ya afya ya msingi ya kukidhi mahitaji ya wananchi. Maeneo mengi ya nchi yana theluthi moja tu au chini ya hapo ya mahitaji yao. Tanzania haina wahudumu wa afya wa kutosha. Shirika la Afya la Dunia linakadiria kuwa Tanzania inahitaji wafanyakazi wa sekta ya afya wasiopungua 92000 wakati wafanyakazi wote waliopo ni 25400. Sera ya serikali ni kuwa na wafanyakazi 140,500 ifikapo mwaka 2019. Vyuo vyote vya afya vinafundisha wafanyakazi 4000 kwa mwaka. Kwa sababu ya mazingira mabovu ya kufanyia kazi asilimia 30 ya wahitimu wote (wafanyakazi 1200) wa sekta ya afya wanaacha kazi mwaka wa kwanza baada ya kuhitimu. Zahanati, Vituo vya afya na hospitali nyingi hazina wafanyakazi wenye ujuzi na ari ya kutoa huduma.

6. Uchambuzi wa mgawanyo wa matumizi halisi ya serikali kisekta yanaonyesha kuwa miaka yote sekta ya afya inatengewa chini ya asilimia 10 ya matumizi yote ya serikali na hakuna dalili ya jitihada zozote za kutenga asilimia 15 ya matumizi ya serikali katika sekta ya afya kama ilivyokusudiwa na sera ya afya ya 2007. Mgao wa matumizi ya serikali katika sekta ya afya umepungua toka asilimia 8.2 mwaka 2008/09 na kufikia asilimia 5.4 mwaka 2010/11.

7. Watanzania wengi bado wanaathirika na maradhi mengi yanayoweza kuzuiliwa kwa gharama ndogo. Vipaumbele vya matumizi ya fedha za serikali viwe katika kinga na tiba ya maradhi ya kuambukiza na kuhakikisha watoto wote wanapata lishe bora. Maradhi yanayohusiana na kupumua, malaria, kuharisha na ukosefu wa lishe bora ndiyo chanzo cha vifo vingi vya watoto. Maradhi haya yanaweza kuzuwiwa kwa gharama ya wastani. Matumizi makubwa ya serikali yanatengwa kuwatibu watu wachache. Gharama kubwa inatumiwa kuwapeleka wagonjwa wachache hasa viongozi nje ya nchi.

Kuhusu suala la Bajeti ya Mwaka 2012-2013

1. Baraza Kuu limebaini kuwa malengo ya bajeti ya 2011/12 hayakufikiwa. Katika hotuba ya bajeti ya juni 2011, ilieleza kuwa “Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wananchi katika kupambana na makali ya maisha. Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12, pamoja na mambo mengine, inalenga katika kuchukua hatua za kurekebisha hali hiyo.” Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa wakati waziri wa fedha anasoma hotuba ya bajeti, mfumko wa bei Juni 2011 ulikuwa asilimia 10.9. Mfumko wa bei uliongezeka na kufikia asilimia 20 mwisho wa mwaka 2011 na umepungua kidogo sana na kuwa asilimia 18.2 mwezi Mei 2012.

2. Mfumko wa bei wa vyakula ni wa juu zaidi. Takwimu za serikali zinaonyesha mfumko wa bei uliongezeka toka asilimia 12 mwezi Juni 2011 mpaka kufikia asilimia 26 mwezi desemba 2011 na Mei 2012 ulikuwa asilimia 24.5. Mfumko wa bei ni matokeo ya matumizi makubwa ya serikali yasiyokuwa na tija. Sekta ya kilimo haijatengewa fedha za kutosha kwa madhumuni ya kuongeza tija na uzalishaji wa chakula na mazao mengine ya kilimo. 

Mgao wa matumizi ya serikali kisekta unaonyesha kuwa sekta ya kilimo ilitengewa asilimia 2.92 mwaka wa fedha 2010/11 na asilimia 1.65 mwaka 2011/12. Taarifa za hali ya uchumi wa taifa zinaonyesha kuwa, kwa muda wa zaidi ya miaka 20 iliyopita, sekta ya Kilimo, misitu na uvuvi kwa pamoja imekuwa inatengewa chini ya asilimia 5 ya matumizi yote ya serikali. Makubaliano ya nchi za SADC ni kutenga alau asilimia 10 ya matumizi ya serikali kwenye kilimo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uzalishaji wa mazao ya chakula na kupunguza umaskini uliokithiri vijijini. 

Sekta ya kilimo imekua kwa asilimia 3.6 wakati ongezeko la watu linakadiriwa kuwa asilimia 2.9. Nafasi muhimu ya serikali katika kuleta mapinduzi ya kilimo ni katika maeneo ya utafiti wa mbegu bora, mbolea inayofaa kwa mazao katika maeneo mbali na madawa ya kuua wadudu, huduma za ugani na elimu kwa wakulima, miundombinu ya umwagiliaji maji na usafiri.

3. Kilimo kipo hoi na bei ya bidhaa za wakulima ikiwemo korosho haiwasaidii wakulima na bado wanaendelea kukopwa kwa utaratibu wa ‘stakabadhi gharani.’ Bei ya pamba imepungua toka shilingi 1100 kwa kilo msimu uliopita na sasa ni shilingi 660/ kwa kilo msimu huu.

4. Katika mwaka 2011/12 Serikali ililenga kukusanya asilimia 17.2 ya pato la taifa kuwa mapato ya serikali. Imefanikiwa kukusanya asilimia 16.9. Ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na mapato yasiyokuwa ya kodi ndiyo hayakufikia kiwango kwa asilimia kubwa. Serikali inalenga kukusanya asilimia 18 ya pato la taifa kama mapato yake. Inakadiriwa kuwa misamaha ya kodi ni asilimia 2.5 ya pato la taifa. Ukwepaji wa kulipa kodi ni asilimia 2-3 za pato la taifa. Sekta ya madini haichaingii ipasavyo katika mapato ya serikali. Serikali makini inaweza kukusanya asilimia 22-25 ya pato la taifa kuwa mapato ya serikali.

5. Sera za kukusanya mapato zimejikita katika kodi za vinywaji na sigara. Sentensi moja inaniudhi kuisikia katika bajeti kila mwaka nayo ni “Ushuru wa “Cigar” unabaki kuwa asilimia 30.” Hivi cigar ngapi zinazovutwa Tanzania mpaka zistahiki kuwa ndani ya hotuba ya bajeti kila mwaka! Bajeti haizungumzii kabisa hatua zinazochukuliwa kuhakikisha sekta ya madini inachangia vya kutosha mapato ya serikali.

6. Katika kukabiliana na upungufu wa umeme serikali iliahidi kuchukua “hatua kadhaa za kukabiliana na upungufu huu, ikiwemo kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 100 Dar es Salaam na ule wa megawati 60 Mwanza.” Katika bajeti ya mwaka huu bado inaeleza “Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa Euro milioni 61 na Benki ya HSBC. Mkopo huu umeelekezwa kugharamia ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa megawati 60 Nyakato Mwanza.” Bajeti tano mfululizo zimekuwa zinaeleza utekelezaji wa mradi huu. Mpaka sasa haujakamilika. Fedha zinazotengwa kila mwaka kukamilisha ufuaji wa umeme, Nyakato Mwanza zinakwenda wapi? Hali ya umeme bado ni tatizo kubwa nchini mbali na mwaka 2008 kutengwa 1.7 trilioni kama mfuko wa kichocheo cha kufufua uchumi (stimulus package) utekelezaji wake hauelezwi uliyeyukia wapi na fedha hizo zilizotengwa zimekwenda wapi! Serikali ya CCM, imeshindwa kutatua tatizo hili na kuisababishia nchi kupata hasara kubwa kwa kudhoofisha uchumi wa nchi. Hali hiyo imezorotesha uzalishaji viwandani na bidhaa zimepanda bei na kusababisha ukali wa maisha kwa watanzania, huduma za mahospitalini, katika sekta ya elimu, upatikanaji wa maji, KUPOROMOKA KWA SHILINGI na mengi mengineyo. CUF tunaamini bila ya umeme wa uhakika nchi haiwezi kupata maendeleo.

7. Serikali pia iliahidi kuweka mazingira mazuri ya kuongezeka kwa ajira. Mpaka sasa tatizo la ukosefu wa ajira ni kubwa mno na halielekei kutatuliwa. Katika nchi yenye nguvukazi ya zaidi ya watu milioni 22, walioajiriwa katika sekta rasmi ya viwanda ni watu 115000 tu.

8. Tatizo kubwa la bajeti yetu ni kuwa matumizi ya serikali hayatekelezi bajeti ya maendeleo iliyopitishwa na bunge. Matumizi ya miradi ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2011/12 yatakuwa chini kwa shilingi bilioni 600 ukilinganisha na bajeti iliyopitishwa na Bunge. Baadhi ya sekta, matumizi halisi ya maendeleo ni chini ya asilimia 50 ya fedha zilizoidhinishwa.

9. Bajeti ya Maendeleo ya 2012/13 ni ndogo. Matumizi yote ya serikali yameongezeka toka shilingi trilioni 13.1 na kufikia shilingi trilioni 15.1 bajeti ya maendeleo imepunguzwa toka shilingi trilioni 4.9 mwaka 2011/12 na kufikia shilingi trilioni 4.5 mwaka 2012/13. Bajeti ya Maendeleo mwaka 2011/12 ilikuwa asilimia 36.4 ya matumizi yote ya serikali. Matumizi halisi ya bajeti ya maendeleo katika mwaka 2011/12 yatakuwa asilimia 33.3. Mwaka 2012/13 Bajeti ya Maendeleo ni asilimia 30 ya bajeti yote. Matumizi ya kawaida yameongezwa kwa asilimia 23.2 na bajeti ya maendeleo imepunguzwa kwa asilimia 8.1. Ukizingatia mfumko wa bei matumizi halisi ya bajeti ya maendeleo yatapungua mwaka 2012/13 ukilinganisha na mwaka 2011/12. Ili kuweka msukumo katika ukuaji wa uchumi bajeti ya maendeleo iwe alau asilimia 40.

10. Matumizi ya kawaida yanakua kwa kasi kubwa kwa sababu ya kuongeza gharama za utawala kama vile kuanzisha wilaya na mikoa mipya, safari nyingi za nje za Rais na viongozi wengine wa serikali, ukubwa wa Baraza la Mawaziri, posho za semina na makongamano. Hatua za maksudi zinahitajiwa kuchukuliwa kubana matumizi ya utawala.

11. Baraza kuu limeshtushwa na hali ya MATUMIZI MABAYA YA FEDHA ZA UMMA kama ilivyoainishwa na taarifa iliotolewa na Msimamizi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Serikali Kuu, halmashauri mbalimbali nchini na mashirika ya umma, mabilioni ya shilingi ya fedha za walipa kodi wanyonge wa Tanzania zimetafunwa na watendaji wachache bila hatua stahiki kuchukuliwa dhidi yao. Baraza Kuu linaitaka Serikali ya CCM na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda kuchukua hatua za kuwakamata wahusika wote waliotajwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Matumizi ya Rasilimali za mafuta, gesi, madini

1. Kuhusu matumizi ya Rasilimali za mafuta, gesi, madini ya uranium na madini mengine nchini, Baraza kuu linaitaka serikali kuweka utaratibu mzuri wa mchakato wa matumizi ya rasilimali hizi ili ziweze kuwanufaisha watanzania wenyewe kwani uzoefu inaonyesha kuwa nchi nyingi dunia zimeingia katika matatizo makubwa kutokana na ufisadi mkubwa wa watu wachache waliohodhi rasilimali hizo kwa maslahi yao.

2. Baraza Kuu la linatoa wito kwa Watanzania wote, pale Tume ya Kukusanya Maoni itapopita kwenye Wilaya zao, kutoa Maoni juu ya sehemu ya Mapato yanayopatikana toka kwenye mauzo ya Mali ya Asili kama vile gesi, dhahabu na madini mengine yagawiwe kwa Wananchi moja kwa moja ili yaweze kupunguza makali ya maisha na kuleta ulinzi shirikishi wa Rasilimali za Nchi na mali ya Asili ya Nchi yetu katika kukuza na kuimarisha dhana ya Utawala Bora.

Mpasuko wa kisiasa ndani ya serikali ya CCM

1. Kuhusu mpasuko wa kisiasa ndani ya serikali ya CCM unaathiri na kuiyumbisha nchi na ustawi wa maisha ya watanzania kwa kiasi kikubwa kutokana na makundi makubwa ya nani awe mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015. 

Jukumu la msingi la chama kinachounda serikali inayounda kufahamu kuwa nchi yetu inahitaji mabadiliko. Baraza Kuu linatoa wito kwa Watanzania kuzinduka na kufahamu kuwa nchi yetu inahitaji mabadiliko. CUF na viongozi wake wako tayari kuwaongoza Watanzania kuelekea katika mabadiliko wanayoyataka. CCM imeshindwa kuiongoza Tanzania. Na tujiandae kuishughulikia kikamilifu mwaka 2014/15 ili CUF iweze kuunda serikali makini itakayoweza kuweka mipango thabiti ya kiuchumi na maendeleo ya Taifa yetu.

Kuhusu suala la Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ZAN ID

1. Baraza Kuu la Uongozi Taifa linaipongeza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar juu ya maamuzi yaliyofanywa na Baraza la Wawakilishi kuhusu kushghulikia suala la Vitambulisho vya mzanzibari mkaazi ZAN-ID. Baraza Kuu linawaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuona haja ya kutatua tatizo hili la Vitambulisho vya Mzanzibar Mkazi ili kuendeleza Ummoja uliopatikana kwa siku za Karibuni.

Kuhusu suala la Sensa

1. Baraza kuu linaitaka serikali kudhibiti utoaji wa Takwimu ili kuepusha migongano isiyo ya lazima ndani ya Nchi. Baraza kuu linaona kuwa mgogoro uliopo sasa baina ya Waislamu na serikali katika suala la Sensa unatokana na serikali kutodhibiti utoaji wa takwimu za idadi ya watu kwa taasisi zisizohusika. Baraza Kuu limesikitishwa na namna serikali imelishughulikia tatizo ikiwemo vyombo vya serikali kutoa takwimu potovu na kuwa na dodoso la sensa linalohesabu nyumba za ibada bila kuhesabu waumini wa madhehebu husika. Linatoa wito kwa Rais Kikwete kukutana na viongozi wa dini zote kuwasikiliza hoja zao na kutafuta maridhiano kuhusu dodoso la dini katika sensa kwani ikiwa sehemu ya jamii itahamasishwa na kususia sensa, zoezi hili lenye gharama kubwa halitafanikiwa na nchi itakuwa na takwimu zisizo sahihi.

Msimamo wa Chama katika mchakato wa kutoa Maoni ya Wananchi kuhusu uandikaji wa Katiba Mpya ya Jamuhuri Muungano

1. Baraza Kuu limewapongeza Viongozi wa Chama kwa jitihada zilizofanyika za kudai Katiba Mpya na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi na kufanikiwa kuishinikiza Serikali kuanzisha mchakato wa kukusanya Maoni ya wananchi juu mabadiliko ya Katiba mpya. Sera ya CUF ni kuwa na Muungano wa Serikali tatu. Sera hiyo imezingatia ukweli kwamba muundo Mpya wa Muungano ndio unaoweza kutoa ufumbuzi wa kudumu kwa changamoto (Kero) za muda mrefu za muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili. Serikali ya Zanzibar iwe na mamlaka kamili ya mambo yake kuhusu Zanzibar. Ikiwemo uamuzi wa mwisho kwa matumizi ya mali asili (Mafuta, gesi na Madini) na matumizi ya kiuchumi ya bahari.

2. Baraza kuu limeona ni vizuri Serikali ya Muungano ihusike na mambo ya jumla ambayo wananchi wa Serikali mbili zinazounda Muungano watakubaliana. Hata hivyo kwa kuwa Muungano sio wa vyama na umekuwepo kabla ya kuungana kwa TANU na ASP1977, na kwa kuheshimu demokrasia ya wananchi wa pande zote mbili (Tanganyika na Zanzibar) waliofanya Muungano uwepo mwaka 1964, CUF- Chama Cha Wananchi kinasisitiza kuwa Tume isikilize na kuyaheshimu maoni ya Wananchi na isiyachakachue.

3. CUF- Chama cha Wananchi tunawahimiza wanachama na wananchi kwa ujumla wao kutoa maoni yao kwa UHURU ili kufanikisha jambo hili kwa mustakabali wa Nchi yetu. Baraza Kuu limesisitiza kusimamia na kuheshimu Sera ya Chama ya kutaka Muundo wa Serikali tatu ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwepo na Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. Baraza kuu linawaomba Watanzania kushiriki kutoa Maoni yatakayowezesha kuandikwa Katiba Bora ikayotujengea Tanzania Tuitakayo.

Kuundwa kwa Tume huru ya Uchaguzi

1. Baraza Kuu linaitaka Serikali kuanzisha Mchakato wa kupata Tume Huru ya Uchaguzi sambamba na Mchakato wa ukusanyaji wa Maoni ya Katiba ili Uchaguzi wa 2015 uweze kufanyika chini ya Tume itayokubaliwa na Watanzania wote ili kuipa muda Tume hiyo kuweza kupitia Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kuhusu suala la Haki ya Kumiliki Ardhi

1. Baraza Kuu la uongozi linatoa wito kwa serikali kuwamilikisha Watanzania ardhi yao hasa ukizingatia mchakato wa soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki na wimbi la kutafuta na kupora ardhi linalofanywa na nchi zenye fedha lakini zinaagiza chakula toka nje. Katiba mpya iwape Watanzania haki ya kumiliki ardhi yao.

Mwisho;

Baraza Kuu la Uongozi Taifa linawatakia watanzania wote ushiriki mwema katika utoaji wa Maoni yatakayowezesha kupatikana kwa Katiba Mpya.



Imetolewa na
Prof.Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti CUF Taifa
HAKI SAWA KWA WOTE

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.