Na Mwantanga Ame
MJUMBE wa Kamati Kuu ya siasa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, Mama Asha Suleiman Iddi, amewataka wanachama wa CCM kuendelea kuiunga mkono serikali yao ili kuiwezesha kupata utulivu na kuweza kuwaletea maendeleo zaidi.
Mama Asha, aliyasema hayo jana wakati akifungua Mkutano wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi kwa Wilaya hiyo katika Afisi ya Jimbo la Kitope Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Mama Asha alisema Chama cha Mapinduzi hivi sasa kina mambo mengi ya maendeleo iliyopanga kuyatekeleza ndani ya kipindi cha miaka mitano na ni vyema kwa wanachama wa CCM kuiunga mkono serikali yao ili iweze kufanikisha mipango hiyo.
Alisema wanachama wa CCM ikiwa watachangia kuvuruga amani ya Zanzibar, wanaweza kujikuta ni wenye hasara baada ya miaka mitano kwani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, atalazimika kuhojiwa alichokifanya katika kipindi hicho.
Kutokana na hali hiyo, Mama Asha alisema ipo haja ya kuona hivi sasa wanachama wa CCM wanampa utulivu Rais na sio kuchangia uharibifu wa amani ya nchi.
“Dk. Shein, ana mengi ya kukufanyieni tumuunge mkono ili kuweza kupata maendeleo yetu tusifanye vurugu kisha ikifika miaka mitano muanze kumnyoshea vidole kafanya nini” alisema Mama Asha.
Mama Asha, alisema wanachama wa CCM wanalazimika kuchukua hatua hiyo kwani hivi sasa imeonekana baadhi ya vijana kuingia katika mkumbo wa vitendo vya vurugu ambavyo vinaweza kuwaingiza katika matatizo.
Kutokana na hali hiyo Mama Asha, aliwataka viongozi wa Jumuiya hiyo kutumia nafasi zao kukaa na vijana kuwaasa ili waache kujiingiza katika vurugu.
Mapema viongozi wa Jumuiya hiyo wakisoma risala yao walieleza Jumuiya yao bado itahakikisha inadumisha amani ya nchi kutokana na hivi sasa kuwepo baadhi ya watu kutaka kuvuruga amani ya nchi.
Walisema kazi kubwa ambayo jumuiya hiyo inatarajiwa kuifanya ni kuhakikisha inasambaza mafunzo kwa vijana juu ya kudumisha amani.
Mapema Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, wilaya ya Kaskazini ‘B’ na Mbunge wa Jimbo la Kitope na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alishiriki katika upigaji kura kuchagua Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi na Wajumbe wengine wa wilaya hiyo.
Uchaguzi huo ulimchagua Hamad Mwinyi kuwa mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, na Katibu ni Abdalla Seif, Katibu Mwenezi ni Hilika Saleh, nafasi ya vijana mkutano wa Wazazi ni Ali Ame, nafasi ya UWT Wazazi ni Cristina Joseph, nafasi ya Wazazi Mkutano Mkuu Wilaya ni Tatu Shida na nafasi ya Mkutano Mkuu Mkoa ni Mwinyi Mahfoudh.
No comments:
Post a Comment