Habari za Punde

Tani 21 za mbegu za mpunga zazalishwa


WIZARA ya Kilimo na Maliasili, imesema imefanikiwa kuzalisha tani 21 za mbegu mpya ya mpunga aina ya NERIKA na kuwapatia wakulima wa Zanzibar.

Waziri wa Wizara hiyo, Suleiman Othman Nyanga, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Matemwe, Abdi Mosi Kombo, aliyetaka kujua ni lini serikali itaanza kugawa mbegu hiyo kwa wakulima wa maweni.

Akijibu hoja hiyo Waziri Nyanga, alisema tangu mbegu hiyo kuanza kuzalishwa tayari kuna tani 21 zilioweza kupatikana na zimegaiwa kwa wakulima wa Zanzibar wakiwemo wa maweni.

Alisema katika kutekeleza hilo, Wizara hiyo pia imeweza kuanzisha vishamba vya maonyesho katika shehia 230 za Unguja na Pemba.

Alisema Wizara hiyo hivi sasa, inapanga kuzalisha mbegu zaidi ya NERICA, katika msimu ujao ili iweze kuigawa kwa wananchi na kuharakisha kuenea kwa mbegu hiyo katika maeneo mbali mbali ya juu ambayo yameonekana kustawi zaidi.

Nae Mwakilishi wa Mtambwe, Salim Abadala Hamad, alitaka kujua kama serikali imefanya utafiti wa kujua kama imepata hasara baada ya kugawa mbegu hiyo.

Akijibu hilo Waziri huyo alisema utafiti umefanywa kwa kina na hivi sasa serikali inaendelea kufuatilia uzuri wa mbegu hizo.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.