Na Khamis Amani
KWA kuzingatia utoaji na ulindwaji wa fursa sawa za haki za binadumu zinapatikana, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina lengo la kujenga Chuo kipya cha Mafunzo.
Chuo hicho ambacho kitakuwa ni cha kisasa, kinatarajiwa kujengwa katika maeneo ya Hanyegwa Mchana wilaya ya Kati Unguja, kitakachoweza kuondosha msongamano wa washitakiwa na rumande wanaohifadhiwa katika Vyuo mbali mbali vya Mafunzo viliopo hivi sasa.
Hayo yameelezwa na Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar Khalifa Hassan Choum, mbele ya Jopo la mahakimu wa mahakama za mkoa, wilaya na mwanzo walioongozwa na Naibu Mrajis wa Mahakama Kuu Ali Ameir Haji, katika ziara ya kukitembelea Chuo cha Mafunzo kiliopo Kilimani Mjini Unguja.
Kamishna Khalifa alisema kuwa, Vyuo vya Mafunzo viliopo hivi sasa hasa cha Kilimani kimekuwa ni hali mbaya kutokana na uchakavu wa jengo lake, na mazingira yake si mazuri.
Alisema kuwa Idara ya Vyuo hivyo vya Mafunzo kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, imeona hali hiyo na kuamua kuliondosha tatizo hilo kwa kujenga Chuo kipya kitakachokwenda sambamba na haki za binaadamu.
Alisema mazingira halisi ya Vyuo vilivyopo hivi sasa si ya kuridhisha, kutokana na Vyuo hivyo kupitwa na wakati huu unaoendana sambamba na haki za binaadamu.
Vyuo vile tumevirithi kutoka kwa wakoloni, mazingira yake bado ni yale yale ya kikoloni japo kuwa tumejitahidi kwa kiasi kikubwa kubadilisha ili yaweze kwenda na haki za binaadamu, lakini pia ipo haja ya kuanzisha Chuo chengine hichi cha Kilimani kiwe cha kihistoria", alisema Kamishna Khalifa.
Kamishna Khalifa alifahamisha kuwa ujenzi wa Chuo hicho kipya unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia hivi sasa mara baada kukamilika kwa hatua za awali za kutafuta mchoro wa Chuo hicho.
Pamoja na hilo, amewaomba mahakimu kuwapunguzia mzigo wa mrundikano wa mahabusu kutokana na kwamba baadhi ya muda wanashindwa kuwamudu hasa katika suala zima la kuwapatia haki zao za lazima.
Alifahamisha kuwa, bajeti wanayotengewa na serikali kwa mwaka kwa ajili ya huduma za wanafunzi na rumande haibadiliki, hata kama wanafunzi na rumande hao wataongezeka hali ambayo inawawiya vigumu katika kumudu utendaji wao wa kazi.
"Mtupunguzie kutuletea rumande, tunashindwa kuwakabili kwa baadhi ya siku kutokana na wingi wao, bajeti huwa haitoshelezi tunayotengewa kwa mwaka ndiyo hiyo hiyo hata tukiwa na wanafunzi na rumande walioongezeka mara dufu", alisema.
Akizungumzia chakula, Kamishna Khalifa alisema kuwa wanafunzi katika chuo hicho wanakula milo mitatu, ambapo asubuhi na jioni hupatiwa chai na mikate na mchana hula wali au ugari kwa maharage.
Chuo cha Mafunzo cha Kilimani, kimejengwa miaka ya 1930 kinakabiliwa na matatizo mbali mbali ya ubovu wa baadhi ya sehemu zake za kuta na uvujaji wa paa, ambacho ndani yake kina jumla ya wanafunzi 82 wakiwemo wanaume 81 na mwanamke mmoja sambamba na rumande 19197 wanaume na wanawake wawili.
No comments:
Post a Comment