RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya aliyepata kuwa Mkuu wa wilaya ya Mbarali, Hawa Ngulume.
Rais Kikwete ametoa taarifa hiyo kufuatia
taarifa za kifo chake kilichotokea katika hospitali ya Jeshi Lugalo, jijini Dar
es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani,
ambapo amefariki jana.
Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete alisema
marehemu Hawa Ngulume katika enzi za uhai wake alikuwa kiongozi shupavu
aliyesimamia maamuzi yake katika majukumu muhimu ya kitaifa kwa lengo la
kuwaletea wananchi maendeleo.
Alisema akiwa akiwa mtumishi wa umma, na
baadaye alipopewa wadhifa wa Mkuu wa wilaya alioutumikia katika wilaya za
Singida Mjini katika Mkoa wa Singida, Kinondoni Mkoani Dar es Salaam na mara ya
mwisho katika wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya.
“Nilimfahamu marehemu, enzi za uhai wake,
kama kiongozi mwanamke shupavu aliyesimamia kikamilifu maamuzi yake, na hivyo
kuthibitisha ukweli kwamba wanawake wakipewa fursa wanaweza”, alisema Rais
Kikwete.
“Kutokana na msiba huo mkubwa,
natuma salamu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa familia ya marehemu,
Mama Hawa Ngulume kwa kuondokewa na mhimili muhimu na kiongozi wa familia. Natambua machungu mliyo nayo hivi sasa kwa
kumpoteza mama wa familia, lakini nawahakikishia kuwa niko pamoja nanyi katika
kuomboleza msiba huu mkubwa”, alisema.
Rais Kikwete aliwataka wanafamilia ya marehemu
wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu wanapoomboleza msiba wa mpendwa
wao kwani yote ni mapenzi yake mola.
Rais Kikwete alimuomba Mwenyezi Mungu, mwingi
wa rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi roho ya marehemu huyo.
No comments:
Post a Comment