Habari za Punde

Vituo vya ununuzi karafuu vyafunguliwa

Na Husna Mohammed
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imefungua rasmi msimu wa ununuzi wa karafuu Unguja na Pemba.

Akitoa taarifa ya serikali kwa vyombo vya habari juu ya ufunguzi wa karafuuu kwa msimu wa mwaka 2012/2013, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui, alisema msimu wa ununuzi unaaza leo kwa wakulima wa Unguja na Pemba.

Mazrui alisema tayari serikali imeanza kuchukua hatua ya kutengeneza vituo vya ununuzi kwa kuweka huduma muhimu za kibinadamu.

Aidha alisema pamoja na mambo mengine lakini serikali itaweka mizani za kisasa katika vituo vya kununulia na katika usafirishaji wa nje kadri itakavyowezekana.

Waziri huyo alisema bei ya kununulia karafuu kutoka kwa wakulima ni shilingi 10,000 kwa kilo moja ambapo kiwango hicho cha bei kitapanda iwapo bei ya kuuzia nje itaongezeka.

"Serikali bado itaendelea kuongozwa na misingi ya kulipa asilimia 80 ya bei ya kuuzia nje kwa msimu ujao", alisema.

Hata hivyo, alisema serikali itachukua hatua zote muhimu za kuhakikisha kuwa ubora wa karafuu za Zanzibar unadumishwa.

Sambamba na hilo, serikali ya Zanzibar imewaomba wananchi wote hasa wakulima wa zao la karafuu kuipa Serikali ushirikiano kama ilivyokuwa katika msimu uliopita ili uvunaji na uuzaji wa karafuu kufanyika katika Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.