MADRID, Hispania
KLABU ya Real Madrid imetwaa taji lake la kwanza la Super Cup nchini Hispania ndani ya kipindi cha miaka minne.
Hatua hiyo inafuatia ushindi wa mabao 2-1 ilioupata dhidi ya Barcelona katika mechi ya fainali ya Super Cup iliyochezwa juzi usiku katika dimba la Nou Camp.
Kufuatia ushindi huo, matokeo ya jumla ya mechi zote mbili, yakawa sare ya magoli 4-4, baada ya Barcelona kushinda pambano la kwanza kwa mabao 3-2 katika uwanja wa Bernabeau, na hivyo Real kuvishwa taji kwa sheria ya goli la ugenini.
Mbali na kichapo hicho, Barcelona ililazimika kucheza pungufu kwa muda mwingi wa mchezo, kufuatia mchezaji wake Adriano kufurushwa nje kwa kuoneshwa kadi nyekundu mnamo dakika ya 28.
Real ilimudu kupachika mabao yote ndani ya dakika 20 za kwanza, ambapo mchezaji Higuain, akitumia makosa ya walinzi wa Barca alitikisa nyavu katika dakika ya 11.
Huku wachezaji wa Barcelona wakijaribu kujipanga na kuanzisha mashambulizi ili kutafuta bao la kusawazisha, Cristiano Ronaldo akagongelea msumari wa mwisho mnamo dakika ya 19.
Dakika chache kabla mapumziko, Lionel Messi akaifungia Barca bao la kufutia machozi kwa mpira wa adhabu, akifumua shuti kutoka umbali wa mita 30.
Katika dakika ya 75, nusura Pedro aifungie Barca bao la pili, lakini shuti lake kali sana liliokolewa na mlinda mlango Iker Casillas.
Wakati mchezo ukielekea ukingoni, timu zote zilipata nafasi za kuongeza mabao, lakini bahati ilikuwa upande wa Real jana kumaliza ubabe wa miaka mitatu mfululizo wa Barca katika taji hilo.
Ushindi huo umeweza kurejesha furaha katika kikosi cha Jose Mourinho, ambacho kilipoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Hispania, La Liga kwa kufungwa 2-1 na Getafe Jumapili. (BBC SPORTS).
No comments:
Post a Comment