HOTUBA YA MHE. BALOZI, SEIF ALI IDDI, MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR WAKATI WA UFUNGUZI WA WARSHA KUHUSU MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI – AWAMU YA TATU YA TASAF, HOTELI YA ZANZIBAR BEACH RESORT, ZANZIBAR, JUMANNE TAREHE 22 -23 JANUARI, 2013Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa,
Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais
Katibu Mkuu, Wizara ya Ustawi wa Jamii, maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto,
Waheshimiwa Wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,
Wakuu wa Wilaya,
Wajumbe wa Kamati za Uongozi wa TASAF, Unguja na Pemba,
Washiriki wa warsha,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Assalaam Alaykum,
Mheshimiwa Mwenyekiti,Awali ya yote, nachukua nafasi hii kuwakaribisha hapa Zanzibar na nategemea mtapata fursa ya kutosha kujadili mada mbali mbali zitakazowasilishwa katika warsha hii na wataalam kutoka TASAF.
Nimefarijika kupata nafasi ya kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa warsha hii muhimu ya kujenga uelewa wa Wadau kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini - Awamu ya Tatu ya TASAF.
Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Wadau wa maendeleo wakiongozwa na Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza na Shirika la Maendeleo la Serikali ya Marekani kwa kukubali kuchangia mpango huu.
Aidha, nachukua nafasi hii, kuwashukuru TASAF ambao ndio waandaaji wa warsha hii na ni mategemeo yangu kuwa washiriki wote mtapata fursa ya kujadili na kuelewa ni jinsi gani Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini utatekelezwa. Michango yenu katika kujadili itasaidia kuboresha utekelezaji wa Mpango huu.
Mwenyekiti,Wote tunakumbuka, kwamba Mpango huu ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 15 Agosti 2012 kule Dodoma. Wakati wa uzinduzi ule Mhe. Rais alionyesha kuridhishwa kwake na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Awamu mbili za TASAF zilizotangulia na akaagiza Awamu ya Tatu ya TASAF iendeleze yale mazuri yote yaliyopatikana pamoja na kuongeza ubunifu kwa jinsi watakavyoweza kuwatambua walengwa wa mpango huu.
Mwenyekiti,Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni zile Kaya Maskini na zilizo katika mazingira hatarishi walioko katika shehia zetu. Kaya hizi zitafaidika kwa kushiriki Mpango wa Jamii wa Uhawilishaji Fedha, Mpango wa Miradi ya Ujenzi ambayo itatoa ajira za muda, Miradi ya ujenzi kwa kutoa huduma za Elimu, Afya na Maji, shughuli za kuweka akiba pamoja na kuwekeza na kujengewa uwezo. Katika muda wa miaka mitano ijayo, Mpango huu unatarajia kuwafikia walengwa wapatao millioni moja na laki tano kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Mwenyekiti,Wanawarsha, mtakubaliana na mimi kuwa wote tumejizatiti kuhakiki kuwa malengo ya Mpango huu yanafikiwa. Ili malengo hayo yafikiwe kwa ukamilifu ushiriki wa wadau wote unahitajika sana. Hivyo, katika warsha hii mtapewa maelezo ya taratibu na miongozo ya utekelezaji stahiki wa Mpango huu. Na hivyo, ni matarajio yangu kuwa mtakwenda kuielezea na kuitekeleza miongozo na taratibu hizo katika maeneo yenu kwa ufanisi mkubwa.
Mwenyekiti, Ningependa kuthibitisha azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuunga mkono utekelezaji wa Mpango huu katika shehia zetu ili kuondoa umaskini kwa manufaa ya Jamii yetu na Taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti,Ni mategemeo yangu kuwa Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini utaimarisha uwazi, uwajibikaji na kutoa fursa kwa makundi mbali mbali kushiriki kwa kutumia mfumo madhubuti wa kubaini walengwa katika Shehia zetu.
Mwenyekiti, Wajumbe wa warsha hii watakuwa na majukumu mbalimbali katika hatua za utekelezaji wa Mpango huu. Hivyo basi, mtumie fursa hii kujadili na kubadilishana uzoefu ili kufanikisha utekelezaji uliopangwa. Baada ya maelezo haya machache, napenda kuchukua nafasi hii kutamka rasmi kuwa warsha hii ya kujenga uelewa wa Wadau kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini – Awamu ya Tatu ya TASAF imefunguliwa rasmi.
Nawatakieni warsha njema na majadiliano yenye mafanikio makubwa katika lengo la kuboresha utekelezaji wa Mpango huu.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment