Habari za Punde

Jussa ataka mafuta,gesi iwanufaishe Wazanzibari


Na Kauthar Abdalla
MJUMBE wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF, Ismail Jussa Ladhu amesema Zanzibar itakapoanza kuchimba mafuta na gesi,uchumi wake utaimarika na kufikia wa nchi ya Qatar ambayo wastani wa pato la mwananchi kwa mwaka ni dola za Marekani 21,000.

Akiwahutubia wanachama wa chama hicho katika viwanja vya Masumbani,jimbo la Chumbuni,Jussa alisema inashangaza kuona serikali ya Muungano inaiwekea ngumu Zanzibar katika suala la mafuta na gesi asilia,wakati upande wa Tanzania Bara wananufaika.

Alisema nchi ya Qatar ambayo haina mafuta, isipokuwa gesi uchumi wake umebadilika na kuwa nchi tajiri katika falme za kiarabu.

Jussa ambae pia ni Mwakilishi wa jimbo la Mji mkongwe alisema sehemu kubwa ya utajiri wa nchi unatokana na viwanda hivyo kutokuwepo kwa viwanda Zanzibar ndio sababu kuu ya kuathirika kwa maeneo ya uchumi.

Aidha alisema suala la mfumko wa bei za bidhaa nchini unaongeza viwango vya riba kwa mabenki kwani uchumi wa kisiwa ni wa kutoa huduma kwa watu wanaopita kibiashara.


Hata hivyo, alisema serikali inajenga mazingira mazuri pamoja na kusimamia sera na sheria zilizopo ili wawekezaji waingie kwa wingi kwa kutambua kwamba mapato mazuri ndio muhimili wa uchumi nchini.

Sambamba na hayo pia alielezea kwamba ni muhimu kufanya kazi kwa pamoja kama nchi bila kujali tofauti za vyama kwani ni vitu vya mpito na nchi itabaki kama ilivyo.

Pamoja na hayo alisema endapo nchi haina utulivu hali ya wananchi iko mashakani ambapo ajira na kipato kwa wananchi hakitakua katika kiwango kinachostahiki.

Juzi Baraza la Biashara la Zanzibar lililokutana chini ya Mwenyekiti wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein lilizungumza kwa kina na kuliwekea maazimio suala la maendeleo ya viwanda kwa uchumi wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.