Na Rose Chapewa, Morogoro
WAZIRI
Mkuu (mstaafu), Edward Lowasa ataongoza shughuli za uzinduzi wa mfuko wa jamii pamoja na tovuti ya chama cha
waandishi wa habari mkoa wa Morogoro (MOROPC) wakati wa sherehe ya kuuaga mwaka
2012 na kuukaribisha 2013.
Hayo
yalibainishwa na Mwenyekiti wa muda wa klabu hiyo,Boniventure Mtalimbo wakati
akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za chama hicho, na kwamba
uzinduzi huo utafanyika Januari 19 mwaka huu katika hoteli ya kitalii ya Nashera mjini Morogoro.
Alisema lengo la kuanzishwa mfuko wa jamii ni
kuwawezesha waandishi wahabari kwenda vijijini kwa ajili ya kuandika habari
kutokana na maeneo hayo kushindwa kufikika kwa urahisi kutokana na ukosefu wa fedha.
Mtalimbo
alisema mbali na waandishi kwenda vijijini pia utakuwa ukisaidia mambo
mbalimbali ikiwemo maafa, kama vile vifo, magonjwa na kuwawezesha kujiendeleza
kielimu.
Akizungumzia
uzinduzi wa tovuti, alisema waandishi wa habari mkoani Morogoro watakuwa
wakiandika makala mbalimbali zikiwemo za kuelimisha jamii,na kuandaa vipindi
vya televisheni na redio na kuingiza kwenye tovuti hiyo.
Aidha Mwenyekiti huyo aliwaomba wadau
mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Morogoro, kujitokeza kuchangia kwa hali na mali
mfuko huo ili kuwawezesha waandishi hao kufanya kazi kwa ufanisi zaidi pamoja
na kuibua mambo mbalimbali yaliyojificha hususani vijijini.
Aliwataja
wadhamini waliojitokeza hadi sasa kuwa ni Hoteli ya Nashera, Benki ya CRDB,
Mamlaka ya Mapato Tanzania,Kampuni ya Umeme ya Mac Dolnad Live line, Kampuni ya
Abood, Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini, Mamlaka ya Maji safi na taka mkoa wa Morogoro (MORUWASA).
No comments:
Post a Comment