Na Zuwena Shaaban, Pemba
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba, Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa amesema miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar yamepata mafanikio makubwa ya kimaendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari afisini kwake, alisema mafanikio ya mapinduzi ya Zanzibar ni ya kujivunia na kuyafurahia kwani yamesaidia kuimarisha maendeleo ya wananchi wake.
Alisema katika sekta muhimu za maendeleo Mkoa wa Kusini umepiga hatua kubwa hasa katika masuala ya ya elimu, afya, mawasiliano,umeme na biashara licha ya changamoto ndogo ndogo zinazokabili sekta hizo.
Alisema sekta ya elimu inakabiliwa na changomoto kadhaa zikiwemo uhaba wa madarasa katika baadhi ya skuli pamoja na kukatishwa masomo wasichana kutokana na kuolewa au kupewa ujauzito.
Katika sekta za afya, alisema tayari Mkoa wake umevuka malengo ya milenia ambapo kila umbali wa kilomita nne kipo kituo cha afya.
Alisema Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya watahakikisha vituo hivyo vinatoa huduma bora za afya kwa wagonjwa.
Aliwahimiza wananchi wa Mkoa huo kushiriki katika shughuli zote za maendeleo katika kipindi hichi cha kuadhimisha miaka 49 ya mapinduzi hayo, ambayo kilele chake kitakuwa Januari 12.
Pia aliwataka kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo kwa kwa kujiepusha kushiriki katika ghasia.
No comments:
Post a Comment