Habari za Punde

Vyama vya siasa visivyo viti vyahoji Mswada wa ruzuku

Na Mwantanga Ame

SIKU kadhaa baada ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kupitisha mswada wa sheria ya ruzuku kwa vyama vya kisiasa, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wameanza kuilalamikia sheria hiyo kwa kudai haina manufaa kwa vyama vyao.

 Malalamiko hayo yamekuja baada ya baadhi ya viongozi hao kudai matakwa yao ambayo waliwahi kuyawasilisha katika vikao vya wadau wa mswada hao na kamati ya kusimamia viongozi wa kitaifa ya Baraza la Wawakilishi. 

Wakizungumza na Zanzibar Leo walisema wanasikitishwa kuona baadhi ya madai ambayo waliyawasilisha katika kikao hicho hayakuweza kuzingatiwa katika baadhi ya vifungu ambavyo walipendekeza. 


 Wakitoa mfano katibu wa chama cha TADEA mjini Zanzibar, Juma Ali Khatib, Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima, Said Soud, walisema mara nyingi vyama ambavyo hushinda katika uchaguzi wa Zanzibar ni CCM na CUF huku vyama vyao hukosa uwakilishi lakini huwa na uwezo wa kupata asilimia za kura.

 Kutokana na kuwepo hilo viongozi hao walieleza mbele ya Kamati walipendekeza kufikiria kuvipa vyama hivyo sehemu ya ruzuku hiyo kwa kuzingatia kura walizozipata kwa vile vyama hivyo bado haviwezi kushika dola kunakosababishwa na CCM na CUF kuwa ndio vyama vinavyopata nafasi za kuchaguliwa. 

 Walisema kuvipa ruzuku hiyo vyama vyao ni sehemu itayoviwezesha kufanya shughuli zao kutokana na kushindwa hata kufanya mikutano ya hadhara ya kuita wanachama wao.

 Walisema suala la demokrasia linahitaji kukuzwa lakini vyama vyao vimekuwa vikishindwa kufanya mikutano ya kuita wanachama wao jambo ambalo limekuwa likiwachangia kufanya vibaya katika chaguzi za serikali. 

 Walisema mfumo uliotumika katika sheria hiyo ya kukubali kuwapa ruzuku hiyo kwa vyama vitakavyokuwa vimeshinda nafasi ya urais, uwakilishi na Diwani huenda ikawa ndoto kwa vyama vyao kufaidika na ruzuku hiyo. 

Walisema ingawa mswada huo ni mzuri kuwepo kwa Zanzibar baada ya ule wa awali kutowanufaisha lakini bado hawaoni kama utakuwa na faida kutokana na vyama hivyo mara nyingi huingia katika uchaguzi vikiwa peke yake. 

Walisema kama serikali ingeweza kuwa pamoja kwa kulifikiria wazo lao wangeweza kuendeleza umoja hata kama pale wangeamua kuungana nao kwa kushirikiana katika chaguzi kwa majimbo ambayo wataona ipo haja ya kuunganisha nguvu zao. 

 Mwenyekiti wa kamati ya kusimamia viongozi wa kitaifa ya Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, akizungumzia juu ya hoja ya viongozi hao, alisema ni kweli walikutana na viongozi hao wa vyama lakini kilichojitokeza mapendekezo yao kushindwa kuzingatiwa kutokana na kuliona suala hilo lingeweza kwenda kinyume na sheria. 

 Alisema fedha zinazotarajiwa kutumika katika ruzuku hiyo ni mali za walipa kodi na haitapendeza kuona zinatumiwa kwa vyama ambavyo haviwezi kutoa wawakilishi wa kuwatetea ama kuwafanyia kazia katika majimbo yao. 

 Alisema pia kuruhusu matumizi hayo kufanyika yanaweza yakasababisha kuwepo kwa utitiri wa vyama ambavyo vitaingia katika uchaguzi na kupata kura lakini kukosa wawakilishi ambapo serikali inaweza kukosa uwezo wa kuvilipa kwa vile sheria imewapa haki ya kulipwa kutokana na kupata kura.

 Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti huyo alisema sheria hiyo itaendelea kubakia hivyo, ila bado wanasubiri kuona mapendekezo yaliyowasilishwa katika sheria ya usajili ya vyama kama itaweza kuvinufaisha vyama vyote vilivyosajiliwa. 

 Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wameipitisha sheria ya ruzuku kwa vya ma na hivi sasa inasubiri kupata ridhaa ya Rais wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.