Habari za Punde

Marekani, CUF, Maimamu walaani mauaji ya Padri Mushi


Na waandishi wetu

MAKAMU  wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amelaani vikali kitendo cha kupigwa risasi na kuuliwa Padre Evaristus Mushi  wa kanisa katoliki Zanzibar.

Alisema kitendo hicho kimevuruga sifa njema ya Zanzibar ya kuwa kisiwa cha amani.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF ametoa kauli hiyo kisiwani Pemba wakati akifungua semina ya madiwani wa CUF inayofanyika ukumbi wa kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi.

Alisema kwa niaba yake binafsi, chama chake na serikali analaani vikali kitendo hicho cha kinyama ambacho kimeitia doa kubwa Zanzibar.

Alisema kitendo hicho ambacho hakikubaliki ni cha kusikitisha kwa vile Wazanzibari wamekuwa wakiishi kwa kuvuliana kwa kipindi kirefu bila ya kutokea vitendo hivyo.


Alisema ni wajibu wa Wazanzibari kuendeleza sifa njema ya Zanzibar kwa kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa kuvumiliana na kuwapa matumaini wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar kwa shughuli mbali mbali ikiwemo ya utalii.

Ameviomba vyombo vya dola kufanya kazi ya ziada kuwatafuta waliohusika na tukio hilo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo, alisema wakati uchunguzi huo ukiendelea kufanyika, ni vyema kwa vyombo vya dola kufanya kazi kwa umakini mkubwa ili kuepuka kuwahusisha watu wasiohusika na tukio hilo.

Amekiri kuwa kitendo hicho ni kikubwa na kibaya, lakini hakijafikia hatua ya kuitangaza Zanzibar kuwa nchi ya kigaidi, na kwamba kufanya hivyo ni kuijengea sifa mbaya Zanzibar na kuwafukuza watalii ambao ndio tegemeo la uchumi wa Zanzibar.

Wakati huo huo Maalim Seif amesema ni lazima maamuzi ya madiwani yaheshimiwe na watendaji wengine katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema madiwani ndio wafanya maamuzi katika serikali ya mitaa, hivyo maamuzi yao yaheshimiwe na watendaji ili kujenga mustakbali mwema katika kuwatumikia wananchi.

Alifahamisha kuwa tatizo lililopo sasa ni kuwa mfumo uliopo unatoa mamlaka makubwa kwa watendaji, hasa makatibu wa Halmashauri na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa.

Alisema wakati serikali imo katika mchakato wa kuleta mageuzi  katika serikali za Mitaa Zanzibar, ni vyema mageuzi hayo yakarekebisha hali isiyoridhisha iliyopo sasa.

Alitoa wito kwa Madiwani  kuchapa kazi kwa bidii na kuhakikisha wanayafahamu, kuyasimamia na kuyatekeleza ipasavyo majukumu waliyokabidhiwa.

Aidha Maalim Seif amewasihi Madiwani wa CUF kutokubali kuburuzwa na watendaji, na kuhakikisha kuwa maamuzi yao katika Mabaraza na Halmashauri yanaheshimiwa na kutekelezwa kwa ukamilifu.

“Endapo Katibu au Mtendaji hafuati maagizo ya Madiwani na anafanya atakavyo, lazima mumuarifu Waziri anayehusika, na kama Waziri atapuuza wasilisheni ripoti kwa Makamu wa Pili wa Rais,” alisema.

Alifahamisha kuwa ili malengo ya utekelezaji yaweze kufikiwa ni vyema kwa Madiwani kufanya kazi bega kwa bega na watendaji wengine wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Masheha, kwa vile kazi na maeneo yao ya kazi yanalingana.

Jumla ya madiwani 83 wa CUF kutoka Pemba na Unguja wanashiriki semina hiyo ya siku 6 ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji inayofadhiliwa na Taasisi ya Friedrich Naumann Foundation (FNF) ya Ujerumani.

Wakati huo huo Marekani imelaani vikali mauaji ya Padrid Evaristus Mushi yaliyofanywa na watu wasiojulikana juzi katika eneo la Beit el Ras mjini Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na Balozi wa Marekani nchiNI Tanzania kwa vyombo vya habari imesema mauaji hayo yanakwenda kinyume na utamaduni wa amani uliodumu katika visiwa hivyo kwa muda mrefu.

Ubalozi huo umesema Zanzibar imekuwa makaazi ya makabila mengi  kutokana uvumilivu na kuheshimiana  walionao wananchi wake.

Taarifa hiyo ilisema vurugu za kidini hazina nafasi nchini Tanzania na popote pale duniani  na kuwataka wananchi wa Zanzibar na Tanzania kukataa vitendo vya chuki vinavyosambazwa na watu wachache  ambao wana lengo la kuvuruga amani, usalama na haiba ya Tanzania.

Marekani imesema iko tayari kuusaidia mfumo wa sheria nchini Tanzania  na kutoa wito  kwa wote waliohusika na mauaji ya Padri huyo kukamatwa, kushtakiwa  na kuhukumiwa kutokana na uhalifu waliotenda kwa viongozi wa dini.

Imewaomba wananchi wa Zanzibar na Tanzania kujenga ustaarabu wa kuvumiliana, busara, umoja  na amani.

Kwa upande wake Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) imelaani vikali kitendo cha mauaji ya Padri Mushi wa Kanisa Katoliki na kusema kitendo hicho si cha kibinaadamu bali ni cha kinyama.

Aidha Jumuiya hiyo ilieleza kushitushwa na kusikitishwa kwake kwa tukio hilo la kikatili na kusema kitendo hicho cha kiharamia kinaashiria kuitia doa Zanzibar ambayo kwa muda mrefu watu wake  wamekuwa wakiishi kwa amani  na ukarimu mkubwa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Katibu wa Jumuiya hiyo, Muhiddin Zubeir Muhiddin ilisema kuwa Maimamu wanaungana na kauli ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa maagizo yake kwa jeshi la Polisi nchini kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini wahusika wa tukio hilo.

Aidha imeliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa uadulifu usioambatana na shindikizo la mtu ama kikundi chochote ili kutambua ukweli bila ya kuwadhuru wasiohusika.

Hata hivyo, JUMAZA iliwataka waumini wa madhehebu yote nchini kuendeleza amani na utulivu na kuwataka kutotoa mwanya kwa watu ama vikundi ambavyo vina nia mbaya ya kutaka kuleta vurugu na kutoelewana kwa wananchi kwa malengo yao binafsi.
Jumuiya hiyo imevitahadharisha vyombo vya habari  vinavyohusisha tukio la kuuawa Padri Mushi na uislamu  na kusema kitendo hicho kinaweza kupandikiza chuki na uhasama katika jamii, hatimae kupandikiza mizizi ya fitna na kulisababishia taifa kuingia kwenye machafuko.
Habari hii imeandikwa na Hassan Hamad, OMKR na waandishi wetu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.