Na Masanja Mabula, Pemba
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi ameonya
tabia ya baadhi ya wananchi kuyafanyia suluhu matendo ya udhalilishaji na unyanyasaji wa wanawake
na watoto wa kike kwa misingi ya kukubalina bila ya kuyafikisha kwenye vyombo
vya sheria.
Akikabidhi baiskeli kwa wahamasishaji wa maendeleo ya
jamii kutoka jumuiya ya wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, alisema kumeendelea
kufanyika suluhu ya matendo hayo hali ambayo inapelekea kuendelea matukio ya unyanyasaji
wa wanawake na watoto.
Alieleza kwamba kila mmoja kwa nafasi aliyonayo anapaswa
kuvikemea kwa nguvu zote vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa wanawake
na watoto na kuitaka jamii kutofanya suluhu bali waviachie vyombo vya sheria
vichukue nafasi yake .
Mkuu huyo wa Mkoa
aliwataka wahamasishaji hao kutoa taaluma kwa jamii ili iweze kutambua wajibu
na umuhimu wao katika kulinda haki za msingi za wanawake na watoto na hivyo
kuongeza wigo katika kupambana na vitendo hivyo.
Aidha alisema bado mfumo dume unaendelea kuwakandamiza na
kuwanyima haki zao za msingi wanawake na watoto, hali ambayo imesababisha
baadhi ya jamii kuona mwanamke kama mtu dhaifu na kumkosesha haki zake kwa
sababu yeye ni mwanamke.
Pia alitumia fursa hiyo kuwatanabahisha wahamasishaji wa
maendeleo ya jamii kuhakikisha kwamba baiskeli walizopewa wanazitumia na kuzitunza
kwa lengo lililokusudiwa pamoja na kuwaeleimisha wanawake wenzao kujiunga jumuiya
hiyo ambayo ina lengo la kuwaendeleza na kuwatoa katika wimbi la umaskini.
Mapema Mratibu wa mradi huo, Nadia Subeti Ali ameitaka serikali
ya Mkoa kutambua kazi wanazofanya pamoja na kuwapa msukumo wa hali na mali
katika kufanikisha majukumu yao ya kutokomeza matendo ya ukatili wanaofanyiwa
wanawake na watoto.
Jumla ya baskeli 50 zenye thamani ya shilingi milioni 6.5
zimetolewa na kukabidhiwa kwa wahamasishaji wa maendeleo ya jamii mkoa wa kaskazini
Pemba ambazo zimetolewa na Jumuiya hiyo kwa ufadhili wa Ashirika la Action Aid.
No comments:
Post a Comment