Habari za Punde

Kubadilishiwa mashtaka Uamsho - Hakimu atupilia mbali ombi la mwendesha mashtaka wa serikali

Na Hassan Ali Ame
 
MPANGO wa kuwabadilishia hati ya mashtaka viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar (Jumiki) umekwama baada ya mahakama kutupilia mbali ombi la upande wa mashtaka katika kesi hiyo.
 
Ombi la kubadilisha hati ya mashtaka liliwasilishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe na mawakili wa washtakiwa na kupingwa vikali na mwendesha mashtaka wa serikali, Mohamed Ali Mohamed, juzi.
 
Akisoma hukumu yake, Hakimu Khamis Jafari, alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili katika kesi hiyo ameona hakuna sababu za msingi za kubadilisha hati ya mashtaka dhidi ya viongozi wa Jumiki, Zanzibar.


Hakimu Khamis alisema kwa msingi huo kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kama kawaida kwa kutumia hati ya mashtaka iliyokuwa imefunguliwa mwanzo Aprili mwaka jana. “Sioni sababu za msingi za kubadilisha hati ya mashtaka baada ya kusikiliza hoja za pande mbili katika kesi hii,” alisema.
 
Hata hivyo mwendesha mashtaka, Mohamed Ali Mohamed, hakukubaliana na uamuzi huo na hivyo kukusudia kukata rufaa kupinga uamuzi huo.
 
Washtakiwa saba katika kesi hiyo wamefunguliwa mashtaka ya kufanya mkusanyiko usio halali kinyume na sheria Na. 6 ya mwaka 2004 ya mwenendo wa makosa ya jinai ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
 
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, viongozi hao wanadaiwa kuwa saa 6.30 mchana wa Mei 26 mwaka jana walifanya mkusanyiko usio halali na kuandamana kinyume cha sheria. Washtakiwa hao ni Sheikh Farid Hadi Ahmed, Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Abdalla Saidi Ali Fikirini Majaliwa Fikirini, Mbarouk Saidi Khalfan, na Haji Sadifa Haji.
 
Washtakiwa hao wanatetewa na wakili mkongwe wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Salum Toufiq na Abdalla Juma ‘Kaka’, ambapo kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Machi 28, mwaka huu.
 
Chanzo - Tanzania Daima

1 comment:

  1. Ndugu muandishi,

    Paragraph zako mbili za mwanzo zinatatanisha.

    Ya kwanza inaonyesha ombi la kubadilisha hati za mashtaka limetolewa na muendesha mashtaka; ya pili inaonyesha ombi hilo limetolewa na mawakili wa washtakiwa. Sasa ni lipi sahihi?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.