Habari za Punde

RPC awashukia wanaopiga waamuzi

 
Na Abdi Suleiman, Pemba
ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Hassan Nassir Ali, amekemea tabia za baadhi ya wachezaji soka kuwapiga waamuzi wanaochezesha ligi za madaraja mbalimbali kisiwani Pemba.
Amesema kwa kipindi chote alichokaa mkoani humo, matukio mbalimbali ya kupigwa waamuzi yamekuwa yakitokea hali aliyosema inarudisha nyuma soka la Pemba.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi wa ligi za madaraja mbalimbali mkoani humo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kamanda huyo alisema, pamoja na kuondoka katika mkoa huo, hatavifumbia macho vitendo hivyo.
Amesema, kwa kuzingatia kuwa lengo la michezo si uhasama bali ni kujenga urafiki, umoja na upendo, hatasita kumchukulia hatua kali za kisheria, mtu yeyote atakaebainika kujihusisha na vitendo vya vurugu ikiwemo kupiga waamuzi.
Alieleza kusikitishwa kwake na vitebndo hivyo, akihoji waamuzi wamekosa nini hata washushiwe vipigo na kuwasababishia maumivu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa ZFA Wilaya ya Chake Chake, Ali Bakar ‘Chifu’, alitaka zawadi hizo ziwe changamoto kwa klabu na wachezaji, kwa kuzidisha ari michezoni.
Katika hafla hiyo, washindi wa ligi daraja la pili Taifa Pemba, timu ya Mkungu malofa, ilikabidhiwa kikombe na shilingi laki tano, huku Wawi Star ikipata kikombe na shilingi laki tatu kwa kuwa washindi wa pili.

2 comments:

  1. Katika hali ya kushangaza juzi kuzifanyia mdahalo muhimu wa wanasheria Zanzibar kuhusu mustakali wa Zanzibar , cha kushangaza naona hata habari moja hujaiweka hapa kulikoni, habari zote ni maskani na rangi ya kijani tu tupatie kila habari muhimu kwa Zanzibar usibague.

    ReplyDelete
  2. Wambieni mzalendo waweke si lazima mapara awake kila kitu na km hupendi tusche sisi wapenzi aw blog isiyo na fitina wala kubaguwa na kuchochea km blog zebu maisha si anzisha yako uweke unavyotaka!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.