Habari za Punde

Mafunzo ya Uchambuzi wa Bajeti kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Na Himid Choko, BLW.SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inastahiki kupongezwa kwa kufanikiwa kutimiza baadhi ya malengo ya Maendeleo ya Millenia ( Millenium Development Goals- MDGs) .

Baadhi ya malengo hayo ambayo SMZ imepiga hatua kubwa ni pamoja na Upunguzaji vifo vya watoto na akinamama wajawazito hatua ambayo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na mafanikio ya Mradi wa Malaria hapa nchini.

Hayo yameelezwa na Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu, Maalim Mohammed Jiddawy wakati akiwasilisha mada kuhusiana na Uchambuzi wa Bajeti katika mafunzo ya kuwajengea Uwezo waheshimiwa wajumbe wa Baraza la Wawakiishi yalifanyika katika Hoteli ya Diomond Dream of Zanzibar , Pwani Mchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Maalim Jiddawy amesmea, hayo ni mafanikio makubwa ambayo yamepelekea kuimarika kwa afya za wananchi na ubora wa utendaji kazi hapa nchini.

Amesema mafanikio ya mradi huu yanapigiwa mfano katika nchi za Afrika ambapo Malaria yamepunguwa kutoka asilimia 25% mwaka 2005 hadi chini ya asilimia 1% mwaka 2012.

Hata hivyo Jiddawy ameelezea wasi wasi wake wa kudumu na kuendeleza mafanikio haya katika hali ambayo washirika wa maendeleo wanaondoa misaada yao na kutaka nchi husika ziendeleze wenyewe.

Hivyo Mhadhiri huyo wa Uchumi ameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi kwa ujumla , wajipange vyema na kuweka mikakati madhubuti ya kudumisha mafanikio hayo.

Jiddawy amebainisha maeneo kadhaa ya kutiliwa mkazo wakati wa kujadili bajeti a serikali ikiwemo usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa sekta binafsi ambayo amesema ni muhimu sana katika uchumi na maendeleo ya Taifa.

Amesema jinsia zote mbili zina umuhimu katika kujenga uchumi ulio imara ingawa katika ripoti ya MDGs ya mwaka 2010 inaonyesha lengo hilo limefikiwa lakini bado taarifa nyingi zinaonyesha hali ya wanawake ndio waathirika zaidi katika umasikini.

Kwa upande wa sekta binafsi, Jiddawy amesema Wawakilishi wanapaswa kupima kwa kiwango gani sekta hiyo imeshirikishwa katika kukuza uchumi na maendeleo hasa ongezeko la ajira na upatikanani wa mikopo katika maeneo ya uzalishaji.

Aidha ameshaurikuwa ni muhimu kwa wahehimiwa Wawakilishi kupatiwa taarifa au ripoti za tafiti mbali mbali zinazotolewa na mawizara ili kuwawezesha na kuwapa fursa zaidi ya kuchambua bajeti.

Amekumbusha kwamba Baraza la Wawakilishi (BLW) linajukumu kubwa kwa wananchi wake la kuhakikisha kwamba bajeti inaleta faida kwa watu wote.

Katika kuhakikisha hilo Mhadhiri huyo wa uchumi amelishauri Baraza la Wawakilishi kuzipa uwezo Kamati zake za Kudumu zinapofanya kazi ya kujadili bajeti ili ziweze kuwaalika wataalamu wengine hasa wa uchumi ili watowe michango yao ipasavyo kama Kamati hizo zinavyofanya wakati zinaposhughulikia Miswaada ya Sheria.

Mapema akiwasilisha mada inayohusiana na utaratibu wa kujadili bajeti, Mkurugenzi wa Mashtaka Ibrahim Mzee Ibrahim amewakumbusha Wawakilishi kwamba majadiliano ya bajeti yajikite zaidi katika kuoanisha bajeti inayopendekezwa kuidhinishwa na mikakati ya kiuchumi ya Kimataifa na ya kitaifa.

Ibrahim ambae ni Katibu wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi amesema, kwa upande mwengine mijadala pia inategemewa iweke wazi mafanikio, matatizo na changamoto ziliopo katika uendeshaji wa majukumu ya kila wizara, na pia kuwakilisha maoni, mitizamo, hofu, wasiwasi, malalamiko , kero na matarajio ya wananchi.

Amesema matokeo ya mijadala hiyo yanatarajiwa yawe ni kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utawala wa sheria na kuzuia udanganyifu, matumizi mabaya na upotevu wa fedha za umma.

Aidha ameelezea umuhiu wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hasa wale wasio Mawaziri (Back Benchers) kujitambua kwa kuelewa dhima kubwa iliyokabidhiwa kwao kwa niaba ya wananchi ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma, na wakati wote wakumbuke wajibu wao kwa nchi, majimbo yao, kwa vyama vyao vya siasa na nafasi zao.

Mafunzo hayo ambayo yamedhaminiwa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP chini ya mradi wake wa kusaidia Mabunge na Vyombo vya Kutunga Sheria LSP, pia yamehudhuriwa na Mawaziri, Manaibu Mawaziri , Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu wakuu na yamezungumzia masuala mbali mbali yenye lengo la kuwajengea uwezo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika masuala ya Bajeti.

Bajeti ya serikali kwa mwaka wa 2013/2014 imewasilisha wiki iliyopita na inanza kujadiliwa hii leo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.