Na MAELEZO ZANZIBAR –16/11/2013
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Dokta Ally Mwinyikai ameliomba Shirika la Kimataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za kuimarisha Maeneo ya usimamizi wa Wanyamapori na Maeneo ya Urithi wa Utamaduni kwa kuzishirikisha jamii zilizozunguka maeneo hayo.
Dk Mwinyikai ameyasema hayo katika Kikao cha 37 cha Mkutano Mkuu wa UNESCO Mjini Paris nchini Ufaransa wenye lengo la kutekeleza Mradi wa kuunganisha nguvu ya utamaduni kwa maendeleo endelevu na amani katika muktadha wa ushirikiano wa kikanda.
Amesema kuwashirikisha Wanajamii hasa Vijana katika kutunza Maeneo ya Hifadhi na Urithi wa Utamaduni kutaleta manufaa makubwa kwani Jamii hizo zitaelewa na kuamini kuwa kulinda turufu hizo ni jukumu lao katika maisha yao.
Alieleza kwamba ushirikishwaji wa Vijana katika kutunza Raslimali na Utamaduni ni Mkakati muhimu katika kupunguza matendo ya kihalifu kama vile Ujangili, uporaji, ukataji miti na Migogoro miongoni mwa jamii zinazozunguka Maeneo ya Mbuga na Urithi wa Utamaduni.
Dkt. Mwinyikai ambaye ni kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa UNESCO alisema Tanzania inaishukuru UNESCO kutokana Vipaumbele vyake katika Ulinzi na uhifadhi wa mazingira na kusisitiza dhima ya urithi katika kukuza maendeleo endelevu, maridhiano na mazungumzo baina ya nchi wanachama .
"Tunajua UNESCO katika miaka minne ijayo itajikita zaidi katika kulinda, kuhifadhi na kuendeleza urithi na majadiliano ya kimaendeleo na pia itahusisha vijana kama sehemu ya mikakati mbalimbali ya kukuza maendeleo endelevu, " alibainisha Dkt Mwinyikai.
Alitoa wito kwa UNESCO kusaidia nchi wanachama katika kujenga uwezo wa wataalam wao wa ndani kupata maarifa na ujuzi ambao ni msingi wa kuwepo katika utekelezaji wa Mikataba ya Utamaduni ya UNESCO.
Aidha , alisema kuwajengea uwezo wa Wataalam wa ndani kunaweza pia kutumika kama mkakati wa kuendeleza ushirikiano na wadau muhimu wa Maswala ya Utamaduni kama vile ICOM , ICOMOS , IUCN, ICCROM na INTERPOL.
Katika Mkutano huo Unaondelea Mjini Paris pia kutajadiliwa Mipango ya kimkakati na Bajeti ya Shirika la UNESCO kwa mwaka 2014-2017.
MAELEZO ZANZIBAR –16/11/2013
Nataka kuuliza huyu Mwinyikai kaanza lini kuwa Dokta? Ni dokta wa nini? sijawahi kusikia kuwa alikuwa akisoma? au Dokta wa Open University? Just curious.
ReplyDelete