Bodi ya mikopo yatakiwa kuongeza kasi ya ukusanyaji madeni

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Bodi ya Mikopo wa Elimu ya Juu Zanzibar imetakiwa kuongeza kasi ya ukusanyaji madeni kutoka kwa wahitimu waliokopeshwa na Bodi hiyo ili kuongeza uwezo wa Bodi kutoa mikopo zaidi kwa wanafunzi.

Wito huo umetolewa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akihitimisha Kikao cha Kutathmini Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mwaka 2012/2013 na robo ya kwanza ya mwaka 2013/2014.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo katika bajeti ya mwaka wa fedha uliopita zilihitajika jumla ya shilingi bilioni 7.7 kulipia wanafunzi 1012 wa zamani na wanafunzi wapya 881 pamoja na madeni ya nyuma.

Kwa upande wa mwaka wa fedha 2013/2014 taarifa imeonyesha kuwa Bodi hiyo imeweza kuwadhamini wanafunzi 1,300 tu kati ya maombi ya wanafunzi 2,500 wenye sifa kutokana na ufinyu wa bajeti.

Taarifa hiyo imezidi kuonyesha kuwa pamoja na Bodi hiyo kudai mabilioni ya fedha kutoka kwa wahitimu lakini hadi sasa imekusanya shilingi milioni 209 tu kiwango ambacho ni kidogo sana.

Sambamba na wito huo Mheshimiwa Rais ameiagiza Wizaya ya Elimu na Mafunzo ya Amali kushirikiana na Wizara ya Afya katika kutekeleza mpango wa uchunguzi wa kitaalamu wa afya kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Alibainisha kuwa kutokana na umuhimu wa zoezi hilo na utaalamu unaohitajika Wizara ya Elimu haina budi kurekebisha sera na kubuni mpangomkakati utakaojumuisha mahitaji halisi ya uchunguzi huo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na kuipongeza Wizara hiyo kwa kazi nzuri iliyofanya katika mwaka uliopita aliitaka Wizara kuzipatia skuli zenye maabara wataalamu wa fani hiyo kusaidia na walimu pamoja na wakutubi kwa skuli zenye maktaba.

Halikadhalika aliitaka Wizara kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa majengo ya skuli unaoambatana na matengenezo ya mara kwa mara kadri panapotokea haja ya kufanya hivyo.

Alieleza kuwa haitakuwa jambo jema kwa Wizara kuyaacha majengo ya skuli bila ya matengenezo ya mara kwa mara hadi kufikia hatua ya kutoweza kutumika.

Awali akitoa maelezo ya wizara yake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna alieleza katika mwaka wa fedha uliopita pamoja na kufanikiwa kutekeleza Mpangokazi wake kwa mafanikio lakini bado Wizara ilikabiliwa na changamoto kadhaa.

Hata hivyo alikieleza kikao hicho kuwa Wizara yake katika mwaka wa fedha 2013/2014 imejipanga kukabiliana na changamoto hizo kwa kuchukua hatua mbalimbali.

Miongoni mwa hatua hizo ni kukamilisha ujenzi wa madarasa 500, vyoo na kuzipatia skuli maji safi na salama, kuchonga madawati 10,000 na kuzipatia skuli vitabu vya kiada na miongozo ya walimu.

Aliongeza kuwa hatua nyingine ni kuendelea kuzipatia skuli za sekondari vifaa vya maabara,kuweka utaratibu wa kuwapima wananfunzi hatua kwa hatua kimasomo na kufanya tathmini pamoja na kuwapatia walimu stahiki zao ikiwemo likizo, marekebisho ya mishahara na posho mbalimbali ili kuongeza ari ya utendaji kazi.


Alibainisha kuwa hatua hizo zimelenga katika kuongeza utoaji wa elimu na kuimarisha kiwango cha ubora wa elimu

Post a Comment

Previous Post Next Post