Na Mwajuma Juma, Zanzibar
UONGOZI wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi Kitaifa umesema kuwa katika
mashindano ya kombe la Mapinduzi ya mpira wa miguu wanatarajia
kuwatumia waamuzi wenye beji ya FIFA na kuchukuwa waamuzi kutoka
Tanzania Bara kuchezesha mechi za michuano hiyo.
Katibu wa kamati hiyo Khamis Said aliwaambia waandishi wa habari
kwamba hatua hiyo inalenga kuboresha michuano hiyo kwa kuhakikisha
wanapata bingwa asietokana na mizengwe.
Alisema kuwa si kama hawawaamini waamuzi wao bali wanataka kuhakikisha
haki inafanyika na hakutakuwa na malalamiko.
Katibu Khamis alisema kuwa katika mahindano ya mwaka jana kamati yao
ilipata malalamiko juu ya waamuzi na kuahidi kwamba katika mashindano
ya mwakani hawatorejea makosa hayo.
“Ili kutorejea makosa katika mashindano yajayo tutawatumia waamuzi
wenye beji ya FIFA na wale wanaotambulika Kitaifa na ikiwezekana
kuongeza waamuzi kutoka Tanzania Bara”, aliema.
Hivyo alisema kuwa katika mashindano hayo wanatarajia yatakuwa mazuri
na kuwa mashindano bora ambayo yatatoa bingwa atakaepatikana kwa haki
bila ya kupita mizengwe oyote.