Marekani yaipatia Zanzibar Dola Laki mbili kusaidia Sekta ya Kilimo nchini

  Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar  Affan Othman akizungumza na Ujumbe kutoka Marekani kabla ya kutiwa Saini Msaada wa Ruzuku ya Dola za Kimarekani Laki 2 kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo USAID ili kuinua kipato cha Wakulima Wadogowadogo wa Zanzibar .
 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar  Affan Othman kulia na Mwenzake kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani USAID Tom Hobgood wakitiliana saini ya Msaada wa Ruzuku ya Dola za Kimarekani Laki 2 kwa lengo la kuinua kipato cha Wakulima Wadogowadogo wa Zanzibar.

 Mkufunzi wa Mradi wa Feed the Future kutoka Marekani Mr. Martin akizungumza na baadhi ya Wakulima wa Bonde la Mpunga la Kipange, Donge Kaskazini Unguja ambao walipatiwa Mafunzo ya kilimo cha kisasa kupitia Mradi huo.
Wakulima wa Bonde la Mpunga la Kipange wakimsikiliza Mkufunzi wa Mradi wa Feed the Future kutoka Marekani Mr. Martin hayupo pichani alipofika kuangalia maendeleo yao katika shamba la majaribio kipange.
(Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar).

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar

Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Kimataifa la Maendeleo la USAID imeisaidia Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar Ruzuku ya jumla ya Dola za Kimarekani Laki mbili ili kusaidia maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.

Msaada huo ni mwendelezo wa Juhudi ya Serikali ya Marekani katika kuongeza uzalishaji na kipato cha wakulima wadogo wadogo wa Zanzibar kupitia Mradi wao ujulikano kama "Lisha Kizazi Kijacho"

Akitoa Salamu zake kabla ya kusaini Msaada huo kiongozi wa Mradi huo kutoka Marekani Tom Hobgood amesema wameamua kuendelea kuisaidia Zanzibar kutokana na misaada yao kutumika vizuri na kufikia lengo lililokusudiwa.

Amesema juhudi zilizochukuliwa na Wizara ya Kilimo za kuwajengea uwezo wakulima wadogowadogo zimezaa matunda na hivyo Wakulima waliopewa mafunzo kupitia mradi wa "Lisha Kizazi Kijacho" wamebainisha faida walizozipata ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wao.

Tom ameongeza kuwa Juhudi wanazozifanya kuwasadia Wakulima wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni utekelezaji wa ahadi za Rais Obama aliyotoa wakati wa Ziara yake Afrika mwanzoni mwa mwaka huu ambapo alibainisha kuwa maendeleo ya Sekta ya kilimo ndio suluhu ya kuondoa Umasikini Afrika.

Amefahamisha kuwa Msaada huo Utanufaisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar na Chuo cha Kilimo Kizimbani ili kuweza kupanga utaratibu mzuri wa kilimo cha kisasa kinachozingatia maendeleo ya Sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Affan Othman Said ameishukuru Serikali ya Marekani kwa juhudi zake za kuisaidia Zanzibar hasa katika kuwakomboa Wananchi wa kipato cha chini.

Amesema Kwa muda mrefu wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakilima bila kuzingatia taratibu zinazoendana nawakati na kwamba Msaada huo unaweza kuwa Mkombozi wa Wakulima.

Amesema kupitia Mradi wa "Lisha Kizazi Kijacho" wananchi wamenufaika sana kwa kupata mafunzo ya kutayarisha Vizuri Mashamba yao na kujua Mbegu bora kulingana na eneo husika na hivyo juhudi hizo zinafaa kuendelezwa.

Kupitia Mradi huo Wakulima walijengewa uwezo mzuri wa kutayarisha Mashamba yao vyema na kujua mbegu sahihi kulingana na eneo husika ili kuongeza uzalishaji wao na kuepukana na umasikini.

Akizungumza na Ujumbe wa Marekani Mmoja wa Wakulima waliopatiwa Mafunzo kupitia Mradi wa"Lisha Kizazi Kijacho" Shadhil Hamis amesema Mradi huo umewasaidia sana na kwao umekuwa kama Mkombozi dhidi ya Umasikini.

'"Kwa kweli zamani tulikuwa hatulimi tunajiumiza tu lakini kupitia Mradi huu ndio tunaona faida ya kilimo maana tunatumia mbegu kidogo wakati wa kupanda lakini tunavuna mavuno ya hali ya juu kabisa" Alisema Shadil.

Ameomgeza kuwa kabla ya kupewa mafunzo ilikuwa wanatumia Karibu Kilo 50 za mbegu kutayarisha Shamba la Nusu Eka lakini kwa Sasa wanatumia kilo mbili kasoro na mavuno ni mengi kuliko hata mwanzo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Juma Ali Juma amesema Mradi huo utawawezesha kuandaa Mashamba 40 Unguja na Pemba ambayo yatatumika kuwajengea uwezo Wakulima ili kuinua kipato chao.

Aidha amewaomba Wakulima waliopata mafunzo kuendelea kuyatumia katika shughuli zao na kuwaelekeza Wakulima wenzao ili hatimae Zanzibar iweze kujikwamua na umasikini.

Awali Mradi wa "Lisha Kizazi Kijacho" ulio chini ya Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani USAID ulikuwa unahudumia Vituo vitatu lakini kutokana na Msaada uliotolewa kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar utawezesha kuhudumia Mashamba 40 ambapo Jumla ya Wakulima 5600 watapatiwa Mafunzo ya kilimo cha kisasa.

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

4 Comments

  1. tutahadhari ndugu zangu dunia hii hakupi mtu chochote bure , ndugu kwa ndugu huhasimiana , ukitaka kuvua samaki lazima iwe na chambo kwanza ndio uweze kumkamata samaki , ndoana tupu hata samaki huikimbia. Serikali iwache tabia ya kuomba nje ya nchi na kututia aibu , wao wenyewe wamewekeza mapesa waliowaibia walalahoi kwenye hizo nchi za kigeni , hatuhitaji misaada kutoka nje kama wataacha tabia ya mkono mwepesi. Tunahitaji wawekezaji wa kuingia nao ubia ili faida iwe kwa wote.Kuchua misaada tu ina mambo yake mtakuja kujua baadae

    ReplyDelete
  2. Mchangiaji hapo juu huwezi kuwambia serikali waache tabia ya kuomba wakati huo ni msaada. ujue tu msaada anapewa maskini. World bank wanatoa misaada kwa njia ya loan kwa developed country. World Bank hio hio kupitia organ zake IDA na IFO inatoa soft loan kwa nchi maskin ili zijikwamue kiuchumi. nchi nyingi zinafadika na hizo pesa.
    Pia kuna dhamira maalum kwa small business kupewa kipaumbele ktk organ za kimataifa. Nadhan US wanaloshirika lao binafsi la kusaidia hizo inch maskin.

    Unatakiwa uangalie jambo positively kwanza.

    ReplyDelete
  3. asante ndugu yangu narudia tena hakuna cha bure katika dunia hii kila kitu kina thamani yake , muda utaamua nani yuko sawa na nani hayuko sawa kama tutakuwa hai bado.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Sisemi nani yupo sawa au laa, hata wewe ukitoa sadaka unalengo ndio maana unatoa, kwa hio nakubaliana na hilo ndio maana nikasema think positively.
      Mzungu akikupa dola 10 pia ana lengo.

      Delete
Previous Post Next Post