Na Salim Said Salim
WAKATI nilipokuwa Bagamoyo wiki iliyopita katika kikao maalumu cha Jukwaa la Wahariri, ndipo nchi hii ilipopata mtikisiko mkubwa wa kisiasa kwa baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Muungano kulazimika kujiuzulu na wengine kuwekwa pembeni.
Karibu kila mhariri kule Bagamoyo alionekana kushitushwa na unyama, mateso, ubakaji, ukatili na mauaji yaliyofichuliwa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira juu ya tathmini ya matatizo yaliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili.
Niliwaeleza wenzangu kwamba matukio kama hayo hayanishitui kwa sababu kwa muda mrefu nimekuwa nikiyaona kama mwenendo unaokubaliwa na serikali yetu inayozungumzia amani na utulivu.
Kauli ile ilionekana kuwashangaza wahariri wenzangu kiasi cha baadhi yao kuniona mtu wa ajabu na siyo Salim waliyemfahamu kwa siku nyingi, baadhi yao nikiwa mwalimu wao katika taaluma ya uandishi wa habari ambayo inasisitiza umuhimu wa kuheshimu maisha ya binadamu.
Lakini nilipowaorodheshea matukio mbalimbali ya aina hiyo yaliyowahi kutokea Zanzibar kwa miaka mingi na hata hivi karibuni watu kubambikiwa kesi bandia, ndipo walipoelewa nilichokuwa ninakieleza.
Kwa kweli tofauti iliyopo sasa ni kuwa mambo haya ya kishenzi yamekuwa siku zote yakifanyika Visiwani mchana kweupe na kufumbiwa macho hata na Bunge, lakini kwa vile sasa yametokea Bara ndiyo watu wanaonekana kukasirishwa na kushituka.
Ninakumbuka mwaka 2001 katika mada niliyoiwasilisha Arusha kwenye mkutano wa kimataifa wa taasisi inayosisitiza ukweli na uwazi ya Transparency International kuwa Watanzania waliopo Bara labda wataelewa ubaya wa madhila yaliyokuwa yakifanyika Zanzibar pale watakapoona mambo haya yamepiga hodi Bara.
Nilieleza kuwa kama waliokuwa wakifanya unyama ule Zanzibar wasingedhibitiwa wakati ule, ipo siku Watanzania waliopo Bara watashuhudia unyama kama uliokuwa ukifanyika Zanzibar.
Sasa tunashuhudia kile nilichokitahadharisha Arusha na kuwashangaza wengi wakati ule niliposema nilikuwa sioni fahari kuitwa Mzanzibari wala Mtanzania kutokana na vitendo vya kinyama vilivyofanyika Visiwani.
Wakati ule mbali ya mauaji ya watu wengi wakiwemo wanasiasa mashuhuri wa Zanzibar, watu walikuwa wanapigwa risasi kama mbuzi Visiwani na sasa tunaambiwa walipigwa risasi kama ng’ombe Tanzania Bara.
Zanzibar tuliambiwa risasi zilizoua watu Shuma Mjini, Pemba, zilipigwa hewani, zikateremka ardhini kwa bahati mbaya na kuua watu. Ule ulikuwa unafiki wa hali ya juu na hadi leo serikali haijatoa kauli ya kuwaomba radhi wananchi kwa kutoa taarifa ya uongo.
Kwa muda mrefu ilikuwa kawaida kusikia watu wameingia majumbani usiku kupora na kubaka wanawake.
Tulipokutana Bagamoyo na baadhi ya wale tuliokuwa pamoja Arusha, walinieleza kwamba hawakutegemea Tanzania kushuhudia unyama ule. Niliwaambia wahenga hawakukosea waliposema ukiona mwenzio ananyolewa wewe tia maji.
Kwa bahati mbaya ndugu zangu wa Bara hawakutia maji vichwani mwao, na matokeo yake wamenyolewa vichwa vyao vikiwa vikavu.
Vitendo vya kinyama kama hivi vimeshuhudiwa katika nchi nyingi duniani, zikiwemo zile za majirani zetu, na vinaendelea hasa katika nchi ambazo waliofanya moja kwa moja au kuhusika kwa njia nyingine na unyama huu kutowajibishwa kisheria.
Sasa wakati umefika kwa Watanzania kuacha kuoneana aibu na muhali, na kuweka pembeni siasa zilizopitwa na wakati za kuwa fulani ni mwenzetu, tumetoka naye mbali na ati mzee wake alipigania uhuru au alikuwa kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar. Huu sio wakati wa huruma.
Kama ni suala la huruma basi huyo aliyefanya huo unyama na mauaji angelikuwa wa kwanza kuwaonea huruma hao aliowadhalilisha, kuwatesa na hata kudhulumu roho zao.
Wazanzibari wameshuhudia unyama wa aina nyingi. Wapo waliouawa kwa kupandisha bendera za vyama vyao vya kisiasa, wapo waliofunguliwa kesi bandia ili kuwakomoa na hili bado linaendelea hadi leo, na wapo ambao wanajulikana kubaka watu majumbani na hawaguswi.
Siku hizi wengine hufanya unyama wakiwa wamejifunika uso kama “Ninja” na hawaguswi kwani kufanya hivyo ndiyo kuendeleza amani na utuliu Visiwani.
Watanzania sasa lazima waamue kwamba sheria isimuonee haya anayeivunja na viongozi ndio wawe wa kwanza kuonyesha mfano wa kuheshimu sheria na maisha ya raia. Roho ya binadamu ambaye ni masikini na mnyonge ni sawa na ya tajiri na mwenye madaraka.
Tukiendelea kufumbia macho matusi, kauli za uchochezi, ubaguzi, fitna na wengine kuwa na haki ya hata kuua na kutesa wengine, tutaipeleka nchi hii pabaya na yale tuliyoyasikia kutokea nchi za wenzetu yatatutokea na sisi.
Kwa muda mrefu ubinadamu umekuwa hauheshimiwi Zanzibar na raia wengi wamekuwa hawana haki za kimsingi na sasa tunaona uoza huu unatambaa Bara.
Vitendo vya watu kupigwa mikong’oto Visiwani, na baadhi ya askari kufunika nyuso zao kama “Ninja” wakati wakidhalilisha watu ni mambo ya kawaida. Baadhi ya hawa askari wamekuwa na ujeuri wa aina yake kama vile wanayo haki ya kutesa na hata kuua watu.
Nimezungumzia mara nyingi namna ambavyo watu wengi wa Zanzibar na hasa wenye asili ya kisiwa cha Pemba wanavyonyimwa haki zao za kimsingi za kibinadamu na kuwa kama wakimbizi katika nchi yao. Sasa wanaambiwwa wahame Unguja na waende kwao.
Wapo wahuni wanaowabagua Wapemba na hata kutamka wazi kwamba wafukuzwe Unguja. Huu ni uchochezi wa hali ya juu na wanaofanya hivi hawaguswi kwa sababu ati kwa muda mrefu wamekitumikia kwa uadilifu chama tawala cha CCM na serikali yake.
Zanzibar inapaswa kujifunza na somo lililotolewa na Serikali ya Muungano ambayo haikujali mwenzetu au fulani aliwahi kushika wadhifa gani katika serikali au CCM. Wote waliobainika kuhusika kwa njia moja au nyingine na unyama wa Operesheni Tokomeza Ujangili wamefukuzwa kazi.
Hii ndiyo demokrasia ya kweli na utawala bora. Heko Bunge na heko Rais Jakaya Kikwete. Tuache kuoneana haya na kulindana kwa maovu na asiyetaka kutimuliwa serikalini kwa kufanya unyama, basi aheshimu sheria za nchi na utu wa wananchi.
Kupewa cheo na serikali, iwe cha waziri, kamanda wa polisi, jeshi au Usalama wa Taifa isiwe nongwa na kuwa leseni ya kuonea na kudhulumu watu.
Tanzania Bara imeonyesha njia kwa kufanya uchunguzi wa mauaji na ushenzi uliofanywa kwa wananchi. Zanzibar inapaswa kuiga mfano wa Bunge ili kusafisha uchafu uliotapakaa na kufungua ukurasa mpya wa watu kuelewana na kusameheana.
Vinginevyo, wengi wataendelea kubaki na kinyongo na kuiona Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haiwatendei haki kwa kutowawajibisha wauaji, wabakaji, wanaotesa watu na wanaoichochea jamii ifarakane.
Wakati Zanibar inakaribia kuadhimisha miaka 50 ya mapinduzi, huu ni wakati muafaka wa kufungua ukurasa mpya wa uwajibikaji kwa kuwafungia milango wahuni wote wanaopendelea kuua na kutesa watu na kuhakikisha sheria za nchi zinaheshimiwa na kila mtu.
Zanzibar haina budi kuwaambia wale wanaopenda mauaji, kutesa na ludhulumu watu kwa kuwaimbia nyimbo maarufu ya mapinduzi isemayo “wahame wende kwao (jela) kwa salama na amani wale wasioitakia mema Zanzibar na watu wake.”
Chanzo : Tanzania Daima
maneno yako yameshiba na chengine wenzetu bara wanj uhuru mkubwa wa vyombo vya habari hapa uhuru huo hatuna uhuru wa mawazo tubadilikeni
ReplyDeleteWawakilishi Zanzibar wamefanya kazi kubwa tu ya kufichua uoza na rushwa wanayofanya mawaziri na ripoti kuandikiwa rais Shein lakini ni huyu Shein ndio weak hachukui hatua yoyote anawaogopa hao mawaziri kwa kuwa ni wana CCM. Huyu Shein ndio wa kuiga huu mfano sio wawakilishi kama anavyosema muandishi.
ReplyDeleteSisi tulizani baada ya kuunda hi suki hawa wawakilishi wa tajikaza kumbe utashi na malumbano, yaso faida, ndio kaziyao wenzu kulebara wanajali maslahi ya nchi na wananchi
ReplyDelete