Na Rehema Mohamed, Pemba
WANANCHI 16,656 wa Zanzibar
wamefaidika na mikopo kwa vyama vya ushirika wenye thamani ya shilingi bilioni
1.27, kupitia Idara ya mikopo iliyo chini ya Wizara ya Uwezeshaji kuanzia mwaka
2000-2013.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mratibu Idara ya
Mikopo Pemba, Nd. Humud Rashid Khamis, alisema fedha hizo zilitolewa kwa wilaya
zote 10 kwa lengo la kuwakwamua wananchi na umaskini.
Kati ya fedha hizo,
alisema tayari shilingi milioni 900.93, zimerejeshwa.Akizungumzia
mafanikio ya wajasiriamali hao, Mratibu huyo alisema ni pamoja na kujipatia
fedha za kujiendeleza kimaisha na kurejesha mikopo katika Idara.
Alisema, vikundi vilivyofaidika na mkopo huo ni vile vinavyojishughulisha
na kilimo, bustani za mboga mboga, ufugaji, miradi midogo, viwanda, biashara za
kusindika matunda, sabuni za dawa, vifaa vya utalii, saluni, vyakula, ufumani
wa vikavu na samani.
Hata hivyo, alisema Idara inakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo wanavikundi kutolipa mikopo yao
kwa wakati, uhaba wa fedha na riba inayolalamikiwa na wanavikundi.
Aliwataka wanajamii kujikusanya na kuazisha
vikundi vya ushirika ili kujikwamua na dimbwi la umaskini
No comments:
Post a Comment