Na Joseph Ngilisho, Arusha
ALIYEKUWA Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Goodluck Ole Medeye, alijikuta katika wakati mgumu wakati alipozimiwa kipaza
sauti kanisani, baada ya waumini kukerwa na kitendo chake kutumia muda mwingi
kuhubiri siasa na kujikosha.
Mdeye ambae aliondolewa kwenye Baraza la Mawaziri katika mabadiliko ya
hivi karibuni yaliyofanywa na Rais Kikwete, alionja machungu hayo katika
uzinduzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), usharika wa Sekei
wilayani Arumeru, ambapo ujenzi wake uligharimu shilingi milioni 400.
Katika hotuba yake, Medeye aliwahimiza waumini hao kuchangua kiongozi
anayefaa na sio chama, kwa kuangalia uwezo na utendaji wake wa kazi, huku
akiwasihi Wachungaji kuombea uchaguzi ujao uwe huru na amani.
''Wananchi waangalie mtu kwanza, chama baadae, shida ya siku moja
itawagharimu katika kipindi cha miaka mitano, tumieni fursa ya katiba kupata
kiongozi mwenye uwezo wa kuwaletea maendeleo kama mimi na si
mwingine,''alisema.
Medeye ambaye ni Mbunge wa Arumeru Magharibi, alionya wananchi
kutokubali kuhongwa kwa fedha ama kurubuniwa kwa kitu chochote, huku akiwasihi
Wachungaji wafanye mahubiri yatakayowahamasisha watu wasiuze ardhi zao ovyo
bali watafute wawekezaji.
Pia alipinga hatua ya yeye kuhusishwa na ukabila bali alisema anapinga
ukabila kwa kuwataka wananchi kutobaguana kwa misingi dini na itikadi huku
akitolea mfano mke wake anayetokea mkoani Kilimanjaro (Marangu) akihoji je
amfukuze kwa kuwa yeye si Mwarusha ama Mmasai, kabila atokalo yeye.
Kauli hiyo ilianza kuibua minong'ono kwa waumini waliokuwepo ndani na
nje ya kanisa, huku wangine wakisema kwa chini aondoke.
Hali hiyo ililazimu kamati iliyokuwa ikiratibu shughuli za uzinduzi wa
kanisa hilo kuitana pembeni kwa muda na mmoja wapo alitoa wazo la kwenda kuzima
kipaza sauti kwa muda wa takribani dakika 3, hali iliyomfanya Mbunge huyo
kuamua kuondoka.
Akihutubia wadau mbalimbali katika harambee ya kuchangia fedha za
hospitali ya kijiji cha Kivulul kata ya Olturoto jimbo la Arumeru Magharibi,
iliyofanyika hoteli ya Golden Rose jijini hapa, Medeye alijichanganya na
kujiita Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati
mshereheshaji alipowaita wadau wamshike mkono.
Alitumia muda mwingi kujisafisha kwa kusema Rais anatambua mchango
wake na hivyo hataacha kutatua matatizo ya wananchi.
Medeye ambaye alikuwa mgeni rasmi katika harambee
hiyo, alitumia nafasi hiyo kutoa ufafanuzi wa kuachishwa kazi kama Naibu Waziri
ambapo alisema watu wasihoji kuachishwa kwake.
No comments:
Post a Comment