Habari za Punde

Dk Shein : Nimefurahishwa na jitihada za Uturuki kuimarisha uhusiano wake na Zanzibar

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi wa Uturuki  Mhe,Ahmet Davutoglu alipofika Ikulu Mjini Zanzibar le akiwa na Ujumbe aliofuatana nao.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                             31 Mei, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amefurahishwa na azma ya Serikali ya Uturuki ya kuteua balozi wa heshima na baadae kuanzisha Ofisi ya Ubalozi mdogo Zanzibar kwa lengo la kukuza uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na Uturuki.
 
Akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Bwana Ahmed Davutoglu Ofisini kwake Ikulu leo, Dk. Shein amesema  historia ya uhusiano kati ya Zanzibar na Uturuki imeanzia karne nyingi, hivyo azma ya kufungua ofisi ndogo ya ubalozi Zanzibar ni uthibitisho wa dhamira ya kweli waliyonayo watu wa nchi hiyo kuendeleza na kuimarisha uhusiano wao na watu wa Zanzibar.
 
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Waziri huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa ambayo ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha kunakuwepo na amani na utulivu Zanzibar imepata mafanikio makubwa hivyo kutoa wito kwa wawekezaji wa Uturuki kuitumia fursa hiyo kushiriki katika kujenga uchumi wa Zanzibar kwa kuwekeza mitaji yao katika sekta mbalimbali.
 
Alieleza kuwa ni matumaini yake wawekezaji kutoka Uturuki watatumia fursa ya kuwepo ushirikiano huo mzuri kati ya nchi mbili hizo pamoja na hali ya utulivu na amani iliyopo Zanzibar kuja kuweka vitega uchumi vyao humu nchini.
 
Dk. Shein alimueleza Waziri huyo kuwa uhusiano kati ya Uturuki na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umekuwa wa kindugu na hiyo inadhihirishwa na ziara zinazofanywa mara kwa mara na viongozi wa nchi mbili hizo.
 
Alibainisha kuwa ziara yake aliyoifanya nchini Uturuki mwaka 2011 ambapo alikutana na viongozi mbalimbali akiwemo Raia wa nchi hiyo ilimuwezesha kufanya mazungumzo ambayo yaliweka msingi wa mahusiano ya muda mrefu kati ya Zanzibar na Uturuki katika maeneo ya afya,utalii na uwekezaji.
 
Kwa hiyo, alimueleza Waziri huyo kuwa ni matumaini ya Serikali na wananchi wa Zanzibar kuona kuwa mazungumzo yaliyofanyika wakati wa ziara hiyo yanafanyiwa kazi kwa wakati muafaka. 
 
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Uturuki kwa misaada yake ambayo imekuwa ikiipatia Zanzibar ikiwemo sekta za afya na elimu.
 
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Bwana Ahmed Davutoglu amesema angependa kuona wawekezaji kutoka Uturuki wanatumia fursa ya kuwepo kwa uhusiano mzuri kati ya nchi hiyo na Zanzibar kuwekeza Zanzibar na kuongeza ushirikiano katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
 
Amesema uhusiano wa Uturuki na Zanzibar ni wa kihistoria hivyo Serikali ya Uturuki imekuwa ikifanya jitihada za kuona uhusiano huo unaimarika siku hadi siku kwa kupanua maeneo ya ushirikiano yakiwemo ya huduma za jamii, uchumi na biashara.
 
Kwa hiyo alimueleza Rais kuwa nchi yake katika hatua za awali inafikiria kumteua Balozi wa heshima hapa Zanzibar na baadae kuanzisha Ubalozi mdogo ili kurahishisha mawasiliano kwa azma ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi yake na Zanzibar.
 
Waziri Davutoglu alisema hatua ya nchi yake kufungua ubalozi wake nchini Tanzania inaonesha namna inavyothamini uhusiano wake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na imekuwa kila wakati inahakikisha uhusiano huo unakuwa imara kwa manufaa ya watu wa nchi yake na Tanzania.
 
Alisema ni matumaini yake kuwa Tanzania nayo itafungua ofisi ya ubalozi nchini kwake kwa nia na dhamira ile ile ya kudumisha udugu na urafiki wa nchi mbili hizo na watu wake.
 
Waziri huyo alimhakikishia Rais wa Zanzibar kuwa nchi yake itaendelea kuziunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kujiletea maendeleo kwa kuendelea kuipatia misaada katika sekta za elimu na afya na kuitaka Serikali kuainisha maeneo ya mafunzo ambayo ni kipaumbele ili yaweze kuzingatiwa wakati wa kutoa fursa za masomo.
 
Bwana Davutoglu ameeleza kuwa katika kuhakikisha nchi yake inakuza ushirikiano katika biashara na utalii inaangalia uwezekano wa shirika la ndege la nchi hiyo kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Uturuki na Zanzibar.
 
Alibainisha kuwa Uturuki imepiga hatua kubwa katika biashara ya utalii kwa kuingiza watalii wapatao milioni 40 kwa mwaka huku waturuki wapatao milioni 8 wakifanya safari za kitalii kila mwaka katika nchi mbalimbali ulimwenguni.
 
Alisisitiza kuwa Zanzibar inahitaji kuweka jitihada katika kutangaza vivutio vyake vya kitalii kwa kuwa yenyewe ni nchi inayojulikana sana ulimwenguni hivyo inachotakiwa kufanya ni kuweka mikakati madhubuti katika kutangaza vivutio vyake katika maonesho ya biashara ya utalii yanayofanyika ulimwenguni.
 
Kwa upande Waziri Davutoglu aliahidi kuyahimiza makampuni ya biashara ya kitalii kufanya ziara Zanzibar kujionea mazingira ya utalii ili yaweze kutangaza utalii wa Zanzibar kwa wateja wao ulimwenguni.
 
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa viongozi mbali mbali wakiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Afya Mhe. Juma Duni Haji na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.