Habari za Punde

Mahakama ya ardhi haina mahakimu

Na Masanja Mabula
MAHAKAMA ya ardhi Zanzibar bado inakabiliwa na upungufu wa mahakimu wa kuendesha kesi za ardhi sambamba na ukosefu wa majengo ya kufanyia kazi.

Hali hiyo imesababisha mrundikano mkubwa wa kesi za ardhi katika mahakama mbali mbali Unguja na Pemba.

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, amesema kwa sasa Zanzibar ina jumla ya mahakimu watano wa mahakama ya ardhi ambao hawawezi kukidhi haja ya kusikiliza kesi za ardhi zinazofikia zaidi ya 1000.

Jaji Makungu aliwaambia wasaidizi wa sheria wa majimbo wakati wa kongamano la wasaidizi wa sheria wa maajimbo Tanzania lililofanyika mjini Unguja.

Alisema pamoja na idara ya mahakama kuchelewesha uamuzi wa kesi hizo, wasaidizi wa sheria wa majimbo wanalo jukumu la kuwaelimisha viongozi wa serikali za mitaa kutojihusisha na migogoro ya ardhi kwa kuwa viongozi hao ndio chanzo cha migogoro hiyo.


“Tatizo ni upungufu wa mahakimu wa mahakama hizo, kwani kwa sasa tunao mahakaimu watano tu kwa Unguja na Pemba hivyo inawawia vigumu kuhudumu kusikiliza kesi zote zinazoripotiwa,” alisema.

Aliwalaumu viongozi wa serikali za mitaa wakiwemo  masheha na madiwani kwa kujihusisha na masuala ya kuuza ardhi, hivyo inakuwa vigumu kuweza kupatikana kwa ushahidi wa kesi hizo mahakamani.

“Unajua kiongozi wa serikali ya mtaa (sheha) unapomwita mahakamani kutoa ushahidi anakwambia niko kikaoni kwa Mkuu wa wilaya au nimeitwa na Mkuu wa mkoa, hivyo ushahidi unakuwa haupatikani,” alisema.


Hata hivyo wasaidizi wa sheria wa majimbo waliitaka idara ya mahakama kuongeza watendaaji wa mahakama ya ardhi ili kuzifanya kesi hizo zipatiwe uamuzi unaofaa  na kwa wakati.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.