Na Fatina Mathias, Dodoma
WAKAZI wa kata ya Mnadani manispaa ya
Dodoma, wamelazimika kutumia mti wa ofisi ya Ofisa Mtendaji kata hiyo, kama kliniki ya kuwapimia watoto uzito kutokana na kukosekana zahanati.
Hayo yalibainishwa jana na Diwani wa kata
hiyo,Steven Masangia,alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alikiri wakazi hao kukabiliwa na
changamoto hiyo na kufafanua kuwa tayari eneo la kujenga zahanati limepatikana.
Alisema eneo hilo ni kubwa lenye uwezo wa kujengwa hata
kituo kikubwa cha afya lakini bado fedha hazijapatikana kutekeleza mradi huo.
"Kata yangu haina zahanati,tunatumia
pale ofisi ya kata kuna mti ambao mzani unatundikwa na watoto wanapimwa
uzito," alisema.
Aliiomba serikali kuchangia ujenzi wa
zahanati hiyo itakayogharimu shilingi milioni
126 ili kwa sababu kina mama wanapata shida.
"Wananchi wangu wamejitahidi
kuchangia kwa hali na mali mpaka sasa tumeweza kufikia hatua ya kumwaga jamvi
chini, walileta fedha,kokoto,mchanga na vitu vingine mpaka tumefikia hatua hii,”
alisema.
Aidha alisema halmashauri imekubali
kuchangia shilingi milioni 20, lakini hata hivyo bado fedha zinazohitajia ni
nyingi.
Akizungumzia maendeleo ya kata hiyo,
Diwani huyo aliwaasa wananchi kutoiachia serikali ifanye kila kitu bali washiriki
katika kuleta maendeleo yao .
No comments:
Post a Comment