Habari za Punde

Watumishi Sheria waaswa kupinga unyanyasaj​i kijinsia

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Fanuel Mbonde akifungua mafunzo kuhusu uzingatiwaji na uelewa wa masuala ya jinsia kwa watumishi wa Wizara hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. 
 Mkufunzi wa Masuala ya Jinsia na Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani  (TAWJA) Jaji Mstaafu Eusebia Munuo akiongea wakati wa mafunzo kuhusu uzingatiwaji na uelewa wa masuala ya jinsia kwa watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria jijini Dar es Salaam mwishoni mwaka wiki.

Mkufunzi wa Masuala ya Jinsia na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Nchini  (TAWJA) Jaji Engera Mmari Kileo akiongea wakati wa mafunzo kuhusu uzingatiwaji na uelewa wa masuala ya jinsia kwa watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria jijini Dar es Salaam mwishoni mwaka wiki. (Picha na Wizara ya Katiba na Sheria).

Na Mwandishi Wetu

Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria na watumishi wa umma kwa ujumla wametakiwa kuwa chachu ya mabadiliko yatakayoondoa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo mbalimbali ya kazi.

Akiongea na watumishi hao mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Jaji Engera Mmari Kileo alikumbusha kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia bado vipo katika maeneo mengi ya kazi na kuwa wakati umefika kwa watumishi wa umma kushiriki kikamilifu katika kuvikomesha.

“Vitendo vya matumizi mabaya ya madaraka yanayoambatana na rushwa ya ngono (sextortion) vipo Tanzania na duniani kote, ndiyo maana chama chetu kimeamua kuvisema, kuvikemea na kuvimaliza kabisa,” alisema wakati akiendesha mafunzo kuhusu uzingatiwaji wa masuala ya jinsia yaliyoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Jaji Kileo na Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ), Jaji Mstaafu Eusebia Munuo.

Kwa mujibu wa Jaji Kileo, pamoja na kufanyika katika maeneo ya kazi, vitendo hivyo pia hufanywa maeneo ya vijijini ambapo watu wenye madaraka huyatumia vibaya kwa kushinikiza rushwa ya ngono.


“Wanawake na wanaume huathirika na ‘sextortion’, ingawa kwa kiasi kikubwa waathirika wakubwa ni wanawake,” alisema Jaji Kileo katika mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na watumishi wote wa Wizara ya Katiba na Sheria na kufanyika katika ofizi hizo jijini Dar es Salaam.

Akiongea katika mafunzo hayo, Jaji Munuo alisema Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda kuhusu uzingatiwaji wa haki za binadamu na kijinsia ambayo inalenga kuhakikisha kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinamalizwa.

“Tunapaswa sasa kuona utekelezaji katika maeneo yetu ya kazi, la sivyo haya mambo mazuri yatabaki katika makaratasi tu,” alisema Jaji Munuo ambaye amestaafu hivi karibuni akiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. 
 
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa kukomesha vitendo vya unyanyasaji, Jaji Munuo alisema vitendo hivyo vikiachwa viendelee, kuna uwezekano wanawake wakaacha kuzaa kwa sababu ya kuhofia kutopata muda wa kutosha kuwahudumia watoto mara wanapojifungua.

“Katika baadhi ya nchi za ulaya, wanawake wasomi wamekataa kuzaa na sasa mamlaka zinawaomba wazae na kupewa likizo ya miaka miwili na hata matunzo ili kujenga nguvu kazi,” alikumbusha Jaji Munuo.

Akiongea wakati wa kufungua mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara Ndg. Fanuel Mbonde alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Wizara yake wa kutekeleza maagizo ya Serikali kuhusu uzingatiwaji wa masuala ya jinsia katika mipango ya Serikali.

“Serikali imeagiza taasisi zake kuzingatia masuala ya jinsia katika kila jambo linalotekelezwa, kwa hiyo mafunzo haya ni muhimu ili kuongeza uelewa wa watumishi,” alisema Ndg. Mbonde.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.