Habari za Punde

Zantel: Huduma ya pesa muhimu kwa maendeleo

UONGOZI wa kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, umesema hatua ya kampuni hiyo kushirikiana na kampuni nyingine za Tigo Tanzania na Airtel kuanzisha huduma mpya itakayowezesha wateja kutumiana pesa ni hatua muhimu katika sekta ya fedha na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
 
Makubaliaono ya huduma hiyo yalifikiwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na viongozi wa kampuni hizo tatu.
 
Hatua hiyo ni ya kwanza katika Bara la Afrika kwa washindani katika sekta ya mawasiliano kuamua kushirikiana kuwezesha wateja wao kutumiana pesa baina ya mitandao yao bila mteja kulazimika kubadilisha kadi yake ya simu.
 
Sasa wateja wa mitandao hiyo wataweza kutumia huduma za TigoPesa, Airtel Money au EzyPesa miongoni mwao bila tatizo lolote. Huduma hiyo inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Zantel, Pratap Ghose, alisema hatua hiyo ni muhimu kwa sekta ya fedha nchini kwa kuwa itarahisisha muingiliano zaidi na urahisi wa kutuma na kupokea pesa.
 
Alisema Zantel inajali na imedhamiria kuona kuwa wateja wake wanazidi kufanikiwa katika biashara zao nchini kutokana na ushirikiano huo mpya.
 
“Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wengine wa mawasiliano hapa nchini kuhakikisha kuwa wateja wetu wanaendelea kufaidika na huduma bora,” alisema kiongozi huyo.
 
Kampuni hizo tatu  ziliishukuru kwa Benki Kuu Tanzania (BOT) kwa kuwezesha mchakato wa uanzishaji wa ushirikiano huo kufanikiwa.  Pia walishukuru taasisi za Bill and Melinda Gates na IFC kwa kuwezesha kwa kiwango kikubwa mkakati huo kufanyika.
 
Awali, Meneja Mkuu wa kampuni ya Tigo Tanzania, Diego Gutierrez, alisema wanafurahi kufanya kazi na wenzao wa Zantel na Airtel kuendeleza huduma ya pesa kwa njia simu nchini.
 
 Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Airtel Tanzania, Sunil Colaso, alisema hatua hiyo ni mapinduzi makubwa katika sekta hiyo ambayo watanzania wengi walikuwa wanasubiri.
 
Chanzo : Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.