Na Masanja Mabula,Pemba
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika
skuli ya sekondari ya Limbani, amefariki
dunia papo hapo na wengine watano
kulazwa hospitali ya Wete, baada ya kugongwa na gari katika eneo la Chasasa.
Ajali hiyo ilitokea jana majira
ya saa saba za mchana baada ya gari aina
ya Scudo yenye namba za usajili Z109 BA ambayo ilikuwa ikiendeshwa na dereva
Abrahman Khamis Juma (45 ) ikitokea Chake Chake kuwagonga na kusababisha kifo
cha mwanafunzi huyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi, Katibu wa hospitali ya Wete, Juma Mahamoud Badru, amekiri kupokea maiti
ya mwanafunzi huyo pamoja na majeruhi
wengine watano ambao wanaume ni wanne na msichana mmoja.
Alimtaja mwanafunzi aliyefariki
kuwa ni Haitham Abdalla Hassan (18) ambapo wenzake waliojeruhiwa ni Fatma
Othman Hamad (18) ambae pia ni mwanafunzi wa skuli hiyo, Massoud Said Juma
(42), Ali Ahmed (55), Suleiman Juma Hamad (52) na Bakar Juma Bakar (26) ambao wameumia sehemu za kichwani.
Akithibitisha kutokea kwa tukio
hilo,Kamanda wa polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Shakhan Mohamed Shekhan, alisema tayari majeruhi
Suleiman Juma Hamad, amesafirishwa kwenda Muhimbili wakati Fatma Othman Hamad
amesafirishwa kwenda
hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani.
Akielezea ajali hiyo, alisema baada
ya gari hilo kumgonga mwanafunzi huyo liliacha njia na kueleka upande wa pili
wa barabara na kuwagonga watu wengine.
0 Comments