Habari za Punde

Zeco Fc safarini kuivaa Tanesco


 

Na Mwandishi wetu,

Timu bingwa ya michuano ya mei mosi iliyofanyika mwezi wa tano mwaka jana ZECO FC inatarajia kufanya safari ya kimichezo kuelekea Tanzania Bara na kucheza mechi mbili za kirafiki.

Kikosi cha timu hiyo kilichoshika nafasi ya kwanza na kutwaa ubingwa kwa taasisi mbali mbali za Zanzibar katika kilele cha sherehe za mei mosi kinatarajiwa kusafiri siku ya Alhamis na kupiga ndinga na kuwafundisha ndugu zao wa TANESCO huko Tanzania Bara siku ya Jumamosi ya tarehe 28/02/2015.

Mechi hiyo imeandaliwa ikiwa na lengo la kusherehekea ubingwa walioupata kwa kuibuka kidedea kwa kuzigaragaza taasisi zilizoshiriki mashindano ya mei mosi mwaka jana, vile vile ziara hiyo ina lengo la kuimarisha udugu na ushirikiano wa utoaji huduma ya umeme uliopo baina ya ZECO na TANESCO.

Kabla ya kucheza mechi hiyo na ndugu zao TANESCO, kikosi hicho kinatarajiwa kucheza mechi ya utangulizi itakayopigwa siku ya Ijumaa ya tarehe 27/02/2015 baina ya ZECO FC na kikosi cha timu ya Best Point Hotel Limited iliyopo Dar es Salaam.

Timu hiyo, itaondoka na msafara wa wachezaji pamoja na viongozi wa timu na watendaji wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) na kurejea nyumbani siku ya Jumapili tarehe mosi, mwezi wa tatu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.