Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar 17/04/2015
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Kazi na Utumishi wa Umma Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema ipo haja kwa
wasomi wa kiislamu kuchukua juhudi za makusudi katika kuunga mkono harakati za uanzishwaji
wa Mtaala wa Epistemolojia ya Kiislamu kwani ndio mfumo pekee utakaowawezesha
vijana hao kwenda sambamba na mabadiliko yanayoendelea kutokea kila siku Duniani.
Ameyasema hayo wakati akifungua
Warsha ya siku 3 ya kujadili utungaji wa Mtaala wa Epistemolojia ya Kiislamu wa
masomo ya Vyuo Vikuu uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Kumbumbu ya Abdurahman
Al-Sumait kilichopo Chukwani, Zanzibar.
Amesema Dini ya Kiislamu ni
neema kutoka Allah ambayo hutofautisha moja kwa moja kati ya binadamu na viumbe
vyengine, hivyo ni wajibu wa kila muislamu kuthibitisha hilo kwa kuelewa Nyanja
zote za uislamu zilizofungamana na Quran na Sunna ambavyo ndio misingi mikuu ya
Epistemolojia ya Kiislamu.
Waziri Haroun amesisitiza kuwa
katika kuendeleza vilivyo mtaala utakaojikita katika misingi ya Epistemolojia ya
Kiislamu ipo haja kwa waislamu wenyewe kujifunza na kuelewa kiundani zaidi mafunzo
ya Quran na Sunna za Mtume (S.A.W) kwani kuna utofauti mkubwa kati ya Epistemolojia
ya Kiislamu na Epistemolojia nyengine ambazo hujumuisha mafundisho ya vitabu
vitakatifu pamoja na mawazo ya watu lakini uislamu unatoa elimu zaidi ya hiyo.
Ametanabahisha kuwa kwa sasa
vyuo vingi ulimwenguni hata katika Nchi za Kiislamu vimetawaliwa na mtaala usio
wa kiislamu jambo ambalo hupelekea kuzalisha wataalamu ambao wanakuwa
kimatiriali zaidi na wasio na hofu juu ya kumuogopa Mungu na wanaofanya mambo
kwa kuangalia matashi yao binafsi.
Nae Makamo Mkuu wa Chuo cha Kumbumbu
ya Abdurahman Al-Sumait Prof. Hamed Rashid Hikmany amesema Warsha hiyo ina
lengo la kujadili mambo tofauti yakiwemo; hatua za mchakato wa kuoanisha, hatua
za kutunga mtaala unaozingatia maeneo makuu ya kujifunza yakiwemo ufahamu,
stadi za mazoezi, namna ya kutatua matatizo na stadi za sayansi, mawasiliano,
uongozi, stadi za pamoja, menejimenti ya taarifa stadi na majukumu ya kijamii
pamoja na taaluma na kanuni na stratejia za uhakiki.
Amesema zaidi ya wataalamu
40 wakiwemo wa Vyuo Vikuu, Maprofesa na Watafiti kutokea Vyuo Vikuu 9 vya Nchi za
Afrika mashariki na Chuo Kikuu 1 cha Malaysia wamekutana Zanzibar kwa ajili ya Warsha
hiyo ya siku 3 ambayo imeanza tarehe 17-19 Aprili, 2015 kwa ajili ya kutunga Mtaala
wa masomo ya vyuo vikuu unaoendana na mabadiliko mbali mbali ya dunia yanayojitokeza
hivi sasa.
Prof. Hikmany amefahamisha
kuwa Warsha hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Fikra ya Kiislamu inayoitwa
International Institute of Islamic Thought (IIIT) yenye makao makuu yake nchini
Malaysia kwa kushirikiana na Chuo chake, vikiwemo vyuo vikuu tofauti vinavyoshiriki
ambavyo ni; Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (Tanzania), Chuo Kikuu cha Umma (Kenya),
Chuo Kikuu cha Moi (Kenya), Chuo Kikuu cha Zanzibar, Chuo Kikuu cha Kiislamu cha
Uganda, Chuo Kikuu cha Musa Bin Bique (Msumbiji), Mradi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu
cha Sudan ya Kusini na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Malaysia.
No comments:
Post a Comment