STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 09 Juni, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametaka kuwepo ushirikiano kati ya Makumbusho ya viumbehai ya mjini Berlin na Zanzibar ili kutoa fursa za kufanyika tafiti mbalimbali ya hazina ya viumbehai vilivyopo Zanzibar.
Akizungumza na uongozi wa Makumbusho hayo mjini Berlin jana, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina hazina kubwa ya viumbehai ambavyo havipatikani katika sehemu nyingine duniani lakini inashindwa kufanya utafiti za kina na kuziweka katika kumbukumbu kutokana na ukosefu wa wataalamu katika fani hiyo.
Kwa hivyo aliuambia uongozi huo kuwa Zanzibar iko tayari kuanzisha ushirikiano na Makumbusho hayo kupitia Idara ya Makumbusho na Mambo ya kale ya Zanzibar pamoja na Idara ya Historia na Akiolojia ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).
Katika mnasaba huo, Dk. Shein ameukaribisha rasmi uongozi wa Makumbusho hayo kutembelea Zanzibar mwaliko ambao ulikubaliwa na uongozi huo.
Akitoa maelezo kwa Mhe Rais, Naibu Mkurugenzi wa Makumbusho hayo anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa na Sera ya Sayansi Dk. Christoph Hauser alieleza kuwa atatuma timu ndogo ya wataalamu kutoka Makumbusho hayo kwenda Zanzibar kuangalia namna kuanzisha ushirikiano na Idara ya Makumbusho ili kubadilishana uzoefu na kutoa mafunzo kwa kushirikiana na SUZA.
Aliongeza kuwa Makumbusho yake iko tayari kuisaidia Zanzibar kuiunganisha na taasisi nyingine kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kufanya utafiti na kuziibua meli zilizozama baharini baina ya visiwa vya Zanzibar na sehemu nyingine za mwambao wa Afrika Mashariki wakati Zanzibar ilipokuwa kituo kikuu cha Biashara kwa ajli ya kuzihifadhi.
Dk. Christoph alifafanua kuwa taasisi yake bado inaendelea na utafiti wake nchini Tanzania kuhusu mabaki ya wanyama wa dinaso na wanategemea baada ya kumaliza kipindi cha utafiti kuandaa mkutano mkubwa wa kisayansi.
Aliongeza kuwa dhamira yao ni kuongeza hamasa kwa wananchi kuhusu taaluma hii hivyo kuvutia vijana kujifunza na kupata wataalamu wengi wa kufanya kazi za utafiti na uhifadhi wa historia ya viumbehai.
Akiwa katika makumbusho hayo Dk. Shein alitembelea sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuangalia mabaki ya mnyama dinaso ambaye aligunduliwa pembeni mwa milima ya kijiji cha Tangaguru katika mkoa wa Lindi mwaka 1906.
Kazi ya kuchimbua mabaki ya myama huyo iliyoanza mwaka 1909 na kumalizika mwaka 1913 ilihusisha wanakijiji zaidi ya 5000 ambapo jumla ya tani 250 za mabaki ya mnyama huyo yalisafirishwa hadi mjini Berlin na kuunganishwa mwaka 1937.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Kitabu cha Guiness World Records cha mwaka 2007 kwa mabaki yaliyoyosimama ya mnyama huyo yaliyopo katika makumbusho ya Berlin ambayo yana urefu wa 13.7 kwenda juu ndio kubwa zaidi kuliko yote duniani.
Mapema jana Dk. Shein alitembelea skuli ya Buruno–H- Burgel iliyoko katika mji wa Postdam na baadae kuonana na mabalozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaowakilisha nchi zao nchini Ujerumani.
Dk. Shein anatarajiwa kumaliza ziara yake ya siku nane nchini humu leo kwa kukutana na Chama cha Wafanyabishara wa Ujerumani wanaowekeza nchini Tanzania.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
0 Comments