Habari za Punde

Polisi Pemba watakiwa kuheshimu na kuzitii haki za binadamu

Na Haji Nassor, Pemba                     

WAPIGANAJI wa jeshi la Polisi kisiwani Pemba, wametakiwa kuwa mfano mzuri wa kuziheshimu na kuzitii haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya kuwachapa makofi na mateke, watuhumiwa wanapowakamata.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Kusini Pemba, Shawal Abdalla Ali, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya haki za binadamu, yaliowashirikisha askari wa usalama barabarani 40, kutoka mikoa wili ya Pemba.

Alisema pindi askari akiwa anaziheshimu na kuzitii kwa kina haki za binadamu kuanzia tokea ukamataji, inaweza kujenga misingi imara na endelevu kwa jamii juu ya haki hizo.

Mkuu huyo wa usalama barabarani alieleza kuwa, wapo baadhi ya askari wamekuwa na mikono mepesi kuwatwanga makofi, mateke na kuwanyima haki nyengine mtuhumiwa, jambo ambalo kisheria halikubaliki.

“Sisi askari lazima tuwe mfano mzuri wa kuigwa kwenye eneo hili la kuheshima haki za binadamu, na ndio jamii itajenga nidhamu miongoni mwao katika hilo na kutuamini’’,alifafanua.

Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa usalama barabarani, alisema askari asiefuata maadili ya kazi zake na sheria za nchi, huwa ni mbabaishaji na hupelekea kulivuruga jeshi zima kwenye utendaji.


Mapema Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba Fatma Khamis Hemed, wakati akiwasilisha mada ya ufafanuzi wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, alisema Katiba hiyo imejenga kwa misingi kadhaa.

Aliyataja misingi hiyo ni mamlaka kuwa kwa wananchi, katiba kushika hatamu, mgawanyo wa madaraka, uwakilishi wa wananchi kwenye baraza la wawakilishi, uhuru wa mahakama pamoja na utawala wa sheria.

Hata hivyo alisema suala la kuiwelewa katiba na sheria nyengine ni jukumu la kila mwananchi, sambamba na kujenga mazingira imara ya kuitii.

Nae Afisa Mipango wa Kituo hicho, Siti Habibu Mohamed akiwasilisha mada ya haki za binadamu, alisema haki hizo ni za asili ambapo kila mmoja anakuwa nazo.

Alifafanua haki ya kwanza na ya msingi, ni ya uhai ambapo kama ikiondolewa na nyengine hukatika kutokana na kuondoa msingi mkuu.


Katika mafunzo hayo ya siku mbili, mada kadhaa zilijadiliwa ikiwa ni pamoja haki za binadamu, sheria usalama barabarani, ufafanuzi wa Katiba ya Zanzibar ya mwkaa 1984, ambapo huo ni muendelezo ya mafunzo ya kuwajengea uwezo askari Polisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.