Profesa Said Ahmed akimkabidhi Bwana Yussuf Shoka Hamad nakala ya kitabu chake kipya kiitwacho; ‘Kamwe si Mbali Tena’ nyumbani kwake Limbani, Wete.
Profesa
Said Ahmed na Bwana Yussuf Shoka wakionesha nakala za vitabu vyao walivyoandika
na kukabidhiana leo hii
-
Naye
akabidhi nakala ya kitabu chake kipya kiitwacho; ‘KAMWE SI MBALI TENA’
Na: Salum Msellem
Mwandishi
mashuhuri wa kazi za fasihi ya Kiswahili nchini na mwalimu mzoefu katika midani
ya lugha na fasihi ya Kiswahili, Profesa Said Ahmed Muhammed amepokea nakala
adhimu ya kitabu cha ‘Paka wa Binti
Hatibu’ kutoka kwa mwandishi chipukizi wa tasnia hiyo Bwana Yussuf Shoka
Hamad .
Tukio
hilo lilifanyika leo huko nyumbani kwa Profesa Said, Limbani Wete, Mkoa wa
Kaskazini Pemba wakati mwandishi huyo chipukizi alipomtembelea mwandishi huyo
nguli wa Afrika Mashariki na kujadili mambo mbali mbali yahususyo uandishi na
taaluma.
Katika
makabidhiano hayo, Profesa Said alimshukuru sana Bwana Yussuf Shoka kwa juhudi zake na ujasiri alioonyesha
wa kuandika kitabu hicho ambacho kwa sasa kimejinyakulia umaarufu mkubwa katika
ulimwengu wa Kiswahili duniani.
Akizungumza
kuhusu mapokezi ya kazi yake hiyo Bwana Yussuf alisema, kwa hakika kitabu
kimeuza na kupokelewa kwa kasi kubwa ambapo kwa sasa ameuza nakala nyingi za
kitabu hicho na bado kuna mahitaji makubwa ya kazi hiyo hasa hasa visiwani
Zanzibar.
‘Kwa
hakika nimeshangazwa sana na jinsi jamii ilivyompokea Paka wa Binti Hatibu.
Juzi juzi tu nilikuja na nakala hamsini (50) lakini kwa muda usiozidi siku tatu
niliuza nakala hizo zote. Na hadi sasa
kuna orodha ndefu ya wasomaji wanataka kitabu hicho. Kwa kweli nashukuru sana
na nimeemewa sana na mapokezi ya kazi yangu hii!’ Alisema Bwana Yussuf.
Akizungumza
kuhusu washabiki wake wakubwa na wasomaji wa kazi yake hiyo Bwana Yussuf
alisema;
‘Nimefurahishwa
sana kuona jinsi gani jamii yetu inathamini kazi za waandishi wazawa. Tena hata
kwa wasomaji wasiokuwa wa fani ya fasihi. Kwa mfano, nimeuza nusu ya nakala
zote kwa wafanyakazi wa PBZ, Pemba na zilziobaki kwa wanafunzi na walimu wa
Chuo kikuu Huria cha Tanzania, tawi la Pemba. Kwa kweli nashukuru sana kwa
kuungwa mkono kiasi hiki!’
Pamoja
na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kitabu hicho, Profesa Said alimnasihi
mwandishi huyo chipukizi nchini kutovunjika moyo na changamoto nyingi
zinazomkabili kwa sasa na kumtaka aendelee kuandika na kuielemisha jamii kwa
kadiri ya vile anavyoimulika na kuiakisi kwa minajili ya kuleta mabadiliko na
maendeleo katika jamii ya Tanzania, Afrika Mashariki na Ulimwengu kwa ujumla.
Profesa
pia alimtaka mwandishi huyo anayejulikana zaidi kwa kazi yake ya ‘Paka wa Binti
Hatibu’ kuongeza kasi ya uandishi na kumtaka aisivunjike moyo hata kidogo
katika kukabiliana na shida zilizopo katika tasnia ya uandishi hasa hasa za
uchapishaji.
‘Nasaha
zangu ni kukutaka tu uendelee kuandika kwa kasi hiyo hiyo. Usivunjike moyo
kwani naona unaenda na kasi nzuri kwa sasa.’
Mwandishi
Yussuf Shoka Hamad hadi sasa ameshakamilisha kazi yake ya ‘Paka wa Binti Hatibu’
na sasa anatarajia kuchapisha vitabu vyengine vitano mwaka huu pindipo kazi
hizo zitachapishwa kwa wakati unaofaa.
‘Kwa
kweli kuna msoyoyo mkubwa katika kuchapisha kazi siku hizi. Mchapishaji anaweza
kuchukua mua mrefu sana kukupatia majibu ya muswada wako na hata kuuchapisha.
Hii inarudisha nyuma kidogo kwa kweli’ Alisema Bwana Yussuf Shoka kumwambia
Profesa Said.
Kuhusiana
na kadhia hiyo, Profesa alimtaka Bwana Yussuf kujaribu kuwasiliana na
wachapishaji wengine ili kuharakisha juhudi zake za uchapishaji wa vitabu.
Wakati
huo huo, Profesa Said alimweleza Bwana
Yussuf kuwa hadi sasa ameshaandika vitabu takribani 57 na moja ya kati ya
kitabu chake kinachotamba kwa sasa ni riwaya yake inayokwenda kwa jina la ‘Kamwe Si Mbali Tena’
ambacho pia alimkabidhi Bwana Yussuf Shoka nakala ya kitabu hicho.
Katika
mazungumzo yao, Profesa aligusia nukta mbali mbali zinazohusiana na Elimu na
maendeleo ya taifa pia sambamba nay ale ya uandishi wa vitabu na kupanuka kwa
kiwango cha taaluma nchini.
‘Jamii
ya Watanzania kwa sasa imepanuka kifikra na kimawazo. Ninaposema hivi sikusudii
wasomi tu, bali hata Watanzania wasiosoma wametanuka sana kiupeo kiasi ambacho
kasi ya maendeleo nchini inakuwa kubwa. Hivyo, ni busara kabisa kwa wasomi
kurejea nchini na kushirikiana na wenzao wengine katika kuharakisha maendeleo
hayo!’ Alisema Profesa Said.
Profesa
Said ni mwalimu mstaafu kwa sasa aliyeamua kwa makusudi kurejea nchini kujiunga
na wazalendo wengine katika kusukuma mbele maendeleo ya Taifa ambapo kwa sasa
na kwa nyakati tafauti amekuwa akifundisha katika chuo kikuu cha Taifa (SUZA)
na chuo kikuu kishiriki cha Elimu Chukwani.
Naye
Bwana Yussuf Shoka ambaye ni mzaliwa wa
Wingwi, Wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba ni mhadhiri wa Kiswahili na
Fasihi katika chuo kikuu cha London (SOAS) na pia anafundisha Kiswahili katika
chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza.
No comments:
Post a Comment