Habari za Punde

TRA: Zanzibar kichaka cha kukwepa kodi


Wakati Rais John Magufuli akipambana na wakwepa kodi ili kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa, takwimu za zinaonyesha uwapo wa wafanyabiashara wanaopitisha bidhaa za magendo kwa njia ya panya kati ya mianya 509, Zanzibar inaongoza kwa kuwa na mianya 422,  huku Tanzania Bara ikiwa na mianya 87.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mwenendo wa ukusanyaji wa mapato, matumizi ya mashine za kielektroniki katika ukusanyaji kodi (EFD), kusitishwa kwa bei elekezi na usajili wa vyombo vya moto, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, alisema bidhaa hizo hupitishwa Bandari ya Tanga na Mtwara zikitokea Zanzibar.

Alisema hali hiyo isipodhibitiwa haraka inaweza kusababisha madhara kwa sababu licha ya Bandari ya Dar es Salaam kuchangia mapato kwa kudhibiti wafanyabaishara wanaokwepa kodi katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Magufuli, bado kuna haja ya kuandaliwa mazingira rafiki yatakayowabana wakwepa kodi wanaotumia njia hizo za panya.

Alisema licha ya Bandari ya Dar es Salaam na mashine za EFDs, kuchangia kuongezeka kwa mapato, pia mamlaka hiyo imeboresha mfumo wa udhibiti wa ukwepaji kodi kwa wafanyabaishara hasa katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Magufuli.

“Mianya ya panya ni mingi na inabidi idhibitiwe haraka, tukiangalia mara moja, Zanzibar kuna mianya 422 inayopitisha bidhaa za magendo, wakati Tanzania Bara ni 87, tusiridhike na kiwango hicho kidogo ila iwekezwe nguvu kubwa kumaliza tatizo hilo,” alisema Kidata.Akitoa mchanganuo wa makusanyo ya kodi ya ndani, alisema kwa Februari mamlaka hiyo imekusanya Sh. trilioni 1.040 kwa Tanzania Bara na Visiwani sawa na asilimia 101.18 ya lengo la serikali kufikisha Sh. trilioni  1.028.
Alisema kwa Januari, TRA ilikusanya kiasi cha Sh. trilioni 1.079  kwa Tanzania Bara na Visiwani sawa na asilimia 102 ya lengo la serikali kufikisha Sh.trillioni 1.059.

Alifafanua kuwa kwa kipindi cha Julai mwaka jana hadi Februari mwaka huu mapato yamefika Sh. trilioni 8.569 sawa na asilimia 99 ya makusanyo yote ya ndani.

Kwa mujibu wa Kidata, makusanyo hayo yametokana na ari na udhubutu ambao mamlaka hiyo imeweka katika kusimamia na kuhakikisha inaendelea kuziba mianya ya ukwepaji kodi ma kuweka mazingira  rafiki kwa wafanyabiashara kwa kutumia mifumo mbalimbali.

Naye Kamishna wa  Kodi za Ndani wa TRA, Yusuph Salum, alielezea mikakati ya mamlaka hiyo kwa Machi hadi Juni mwaka huu, kuwa wataendelea  kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, kufichua wakwepa kodi, kupambana na rushwa,   pamoja na kupanua wigo wa kodi kwa kusajili wafanyabishara ambao hawajasajiliwa kama  washereheshaji na wanataaluma.

Kadhalika, alisema TRA itasimamia kwa karibu matumizi ya mashine za EFDs na utoaji wa risiti na itafuatilia na kudai malimbikizo ya kodi kutoka kwa wadaiwa sugu pamoja na kuendeleza ukaguzi wa kodi kwa wafanyabaishara. 

“TRA iko katika mchakato wa mwisho wa kubadilisha mfumo wa kusimamia mapato ya ndani, hivyo kupitia bajeti ya serikali ya 2017/17, kutakuwapo na utaratibu mpya utakaochangia ukuaji wa mapato,”alisema Salum.

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Forodha, Akonary Kaima, aliongeza kuwa matumizi  ya bei elekezi katika mchakato wa uthaminishaji wa bidhaa bandarini ni kinyume cha sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo TRA itaendelea na shughuli za kiforodha kulingana na sheria bila kuathiri eneo jingine.

“Kwa sababu TRA, itadhibiti ukaguzi na uthaminishaji halisi, kila mfanyabaishara anatakiwa kulipa ushuru na kodi kulingana na thamani ya bidhaa husika,”alisema.

Alifafanua kuwa, kuna magari yaliyoingia nchini na kusajiliwa bila kufuata taratibu za forodha na  kusababisha yamilikiwe kinyume cha taratibu, hivyo wamiliki wajisalimishe TRA, kufanyiwa uhakiki ikiwa ni pamoja na kuyalipia kodi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.