Habari za Punde

'Wachezaji, Viongozi Wanapenda Safari Siyo Mchezo' ' Kocha Bushiri'

Kocha mkuu wa kikosi cha KMKM Ali Bushiri amesema maandalizi duni yanayoendelea kufanywa na vilabu vya Zanzibar kwenye mashindano ya Kimataifa itabaki kuwa ndoto kwa timu hizo kufanya vyema.


Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza kufuatia kichapo cha bao 4-0 walichopata klabu ya JKU kutoka kwa SC Villa Jogoo ya Uganda hapo jana kwenye mchezo wa awali wa kombe la Shirikisho barani Afrika.
Bushiri alisema licha ya JKU kuweka kambi mkoani Ruvu jijini Dar es salaam lakini imeonekana kambi hiyo haikuendana na maandalizi ya mchezo huo.
"Inawezekana ukaweka kambi lakini iyendane na umuhimu wa mchezo, lakini leo unaenda kambi unacheza na timu za madaraja ya chini, haiwezekani kufanya vizuri"
Aidha kocha Bushiri aliienda mbali zaidi kwa kudai kuwa timu zote zinazopata nafasi ya kuiwakilisha Zanzibar kwenye michezo hiyo huweka maslahi yao binafsi mbele na siyo taifa.
"Sasa hivi ni kama ada baadhi ya viongozi na wachezaji wakipata nafasi hii basi huangalia sana safari na posho tu na siyo mchezo"
Kwa upande mwengine kocha huyo mzoefu kwenye mashindano ya kimataifa alitoa angalizo kwa viongozi wa ZFA kuwa makini sana juu ya upatikanaji wa bingwa na makamo bingwa wa ligi kuu ya soka visiwani hapa.
Alidai kuwa baadhi ya vilabu hujaribu kufanya mbinu mbadala ili viweze kupata ubingwa na kuwakilisha nchi kwenye mashindano hayo jambo ambalo huliathiri taifa kisoka.
Klabu ya JKU baada ya jana kupokea kichapo hicho cha bao 4-0 kutoka kwa SC Villa Ijumaa ijayo itaikaribisha klabu hiyo uwanja wa Amaan mjini Zanzibar na ili JKU ifanikiwe kusonga mbele inahitaji ushindi wa bao 5-0.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.