Habari za Punde

Wachumaji wa karafuu waliopata ajali walipwa fedia

Na Ali Mohamed
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) Maalim Kassim Suleiman amekabidhi fedha TZS 42 milioni za fidia kwa wachumaji 37 wa zao la karafuu waliopata ajili kwa mwaka 2015/2016.

Akikabidhi fedha hizo katika ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi Chake Chake Pemba, Mwenyekiti huyo alisema kutolewa kwa fidia kwa Wachumaji wanaopata ajali ni juhudi za Serikali ya kuwajali wakulima wa zao la karafuu ambao wanafanya kazi muhimu katika kuendeleza uchumi wa nchi.

Alifahamisha kuwa Serikali kupitia Shirika la ZSTC na Mfuko wa Maendeleo ya karafuu itaendelea na utaratibu huo wa kuwalipa fidia wahanga wa zao la karafuu.

Alisema kuwa sio rahisi kufidia maisha ya watu na maumivu wanayoyapata wachumaji wakati wanapopata ajali lakini utaratibu huo wa kuwapa fidia utasaidia kujenga ari na imani kwa wananchi kushiriki katika zoezi la uchumaji karafuu msimu unapofika.

Aliwataka wakulima kutoitumia vibaya fursa hiyo ya kupata fidia kwa kufanya udanganyifu, hadaa na uongo wa aina yoyote kwa lengo la kupata fedha hizo wakati ambapo mtu hajapata ajali katika harakati za uchumaji karafuu.


Aidha mwenyekiti huyo aliwaasa wazazi na wananchi kwa jumla kutowatumia watoto chini ya umri wa miaaka 18 katika uchumaji wa karafuu kwa vile kazi hiyo ni miongoni mwa kazi ngumu kwa watoto.

Alisema kwa mujibu wa sheria za kimataifa ambapo Tanzania na Zanzibar zinaziheshimu sheria hizo watoto hawatakiwi kuajiriwa au kutumiwa katika kazi ngumu.

Nae Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu Ali Suleiman Mussa alisema kwa mujibu wa makubaliano na Shirika la Bima Zanzibar watoto chini ya umri wa miaka 18 hatozingatiwa katika suala la kupata fidia.

Alisema kuwa Shirika la ZSTC kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu limeingia makubaliano Shirika la Bima Zanzibar kwa kuwakatia bima wakulima wote wanaopata ajali wakati wa uchumaji ili kuwalipa fidia.

Kwa mwaka 2015/2016 kesi zote za wachumaji kupata ajali katika uchumaji ambazo zimeripotiwa ni 133, Pemba 123 na Unguja ni 10 ambapo watu watatu wamekufa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.