STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 10.09.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amekagua matengenezo makubwa ya kuwekwa mpira wa kukimbilia
(Tatan) katika uwanja wa Gombani Pemba na kupongeza hatua iliyofikiwa ambayo itazidi
kuimarisha sekta ya michezo hapa nchini.
Dk. Shein alifika
kiwanjani hapo akiwa ameongozana na viongozi mbali mbali wa Serikali akiwa na
mwenyeji wake Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma ambaye
alimpa maelezo ya kina juu ya maendeleo ya matengenezo hayo makubwa
yaliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika ukaguzi wake
huo, Dk. Shein alisema kuwa kukamilika
kwa uwekaji huo wa Tatan katika uwanja huo wa Gombani Pemba kutauwezesha mchezo
wa riadha kufanyika kwa ustadi mkubwa zaidi sambamba na kuufanya uwanja huo uwe
umekamilika kimichezo hatua ambayo itaendeleza kuibua vipaji vya mchezo huo hapa
nchini.
Alisisitiza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na juhudi za kuimarisha na
kuongeza miundombinu ya michezo katika maeneo yote yaliotengwa maalum kwa
michezo katika visiwa vya Unguja na Pemba ili kuirejesha Zanzibar katika asili
yake kwenye anga ya michezo.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alisisitiza haja kwa uongozi wa Wizara hiyo kuhakikisha eneo lote
lililozunguka uwanja huo linakuwa salama na halivamiwi kwa ujenzi usio rasmi.
Nae Waziri wa Wizara
ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma alimueleza Dk. Shein maendeleo yaliofikiwa
katika matengenezo ya tatan katika uwanja huo wa Gombani pamoja na hatua
nyengine zinazoendelea kuchukuliwa ili uwanja huo uzidi kuvutia kimataifa.
Aidha, Waziri Juma
alieleza kuwa hatua iliyofikiwa katika matengenezo hayo ni nzuri na
kumuhakikishia Dk. Shein kuwa juhudi zaidi zinaendelea kuchukuliwa katika
kuhakikisha baadhi ya maeneo ya uwanja huo yanafanyiwa ukarabati awamu kwa
awamu yakiwemo maeneo ya majukwa ili uzidi kuimarika na kuvuti zaidi.
Matengenezo ya uwekaji
wa tatan hizo yalioanza mwaka 2013 yalifanyika
kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza na ya pili ilifanywa na Kampuni ya Nowe
Investment kutoka Dar-es-Salaam na awamu ya pili ya uwekaji wa tatan ilifanywa
na Kampuni ya Guangzhou Jrace Athletic kutoka China.
Tatan hiyo
iliyozungushwa katika kiwanja hicho mbali ya kuwekwa katika sehemu maalum kwa
kukimbilia pia imeongezwa kwa baadhi ya maeneo katika kiwanja hicho ambayo
yatawezesha baadhi ya michezo kuweza kuchezwa katika kiwanja hicho ukiwemo
mchezo wa vinyoya na michezo mengineyo.
Hata hivyo, uwanja huo
wa Gombani tayari umeshawekewa nyasi za bandia ambazo tayari zimeshaanza
kutumika kwa kuchezewa mashindano mbali mbali ya mpira wa miguu yanayofanyika
kisiwani Pemba.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment