Habari za Punde

Waonyesheni wafanyakazi haki zao: Mdhamini Massoud


Na Haji Nassor, Pemba

AFISA Mdhamini wizara ya Nchi Ofisi ya rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Pemba Massoud Ali Mohamed, amewataka wakuu wa Idara zilizomo ndani ya wizara hiyo, kuwaonyesha haki wafanyakazi wao, na sio kuwakumbusha wajibu wao pekee.


Alisema moja ya kazi kubwa ya wakuu hao wanapokuwa kwenye vikao vyao, ni kuwaleza watendaji wao juu ya haki zao, kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma, badala ya kuwasomea na kurejea mara kwa mara wajibu na majukumu yao.

Afisa Mdhamini huyo, alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na wakuu wa Idara hizo, kwenye mkutano maalum uliofanyika kwenye ukumbi wa wizara hiyo mjini Chakechake.

Alieleza kuwa, ingawa haki kwanza hufuatiwa na wajibu na jukumu la mfanyakazi, lakini wasisahau kuwaleza haki zao, ili wapate nguvu na moyo kwenye utendaji wao wa kazi za kuihudumia jamii iliopo.

Aidha Afisa Mdhamini huyo, alisema suala la kufanya kazi kwa kufuata sheria na maadilini ya utumishi, ndio njia bora ambayo itawaepusha wafanyakazi, kufanya kazi zao za kila siku kwa mazoea.

“Jamani sisi wakuu wa maidara, lazima pamoja na kuwahimiza watendaji wetu kazi, zao lakini pia tuchukue muda kuwaelimisha na kuwatajia kwa kina juu ya haki zao’’,alifafanua.

Akizungumzia kuhusu ushirikiano baina ya taasisi moja na nyengine, alisema ndio njia pekee ambayo itarahisisha kazi zao za kila siku, badala ya kila mmoja kujifungia na kuendesha shughuli zake.

“Mimi naamini mahakama, afisi ya mkurugenzi wa mashitaka, afisi ya wakfu, ZAECA mkifanya kazi kwa kushirikiana, mnaweza kutoa huduma bora na ilio nzuri kwa wananchi wetu’’,alifafanua.

Kwa upande wake katibu wa afisi ya Mufti Pemba sheikh Abrhaman Ali Naam, alisema kutokana na ushirikiano anazo kumbukumbu kwa miaka iliopita kufanikisha vyema majukumu yao.

Nae Mwanasheria dhamana wa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba Ali Rajab Ali, alisema suala la kutoa taarifa kutoka Idara moja kwenda nyengine, lazima liwe na mipaka kutokana na kila Idara kuwa na sheria zake za ndani.

“Mimi sina wasiwasi juu ya kupashana habari, lakini lazima tusisahau kuheshimu sheria za utumishi na katiba jinsi ilivyoelekeza namna ya kutunza siri za ofisi’’,alifafanua.

Katika kikao hicho cha kawaida ambacho kimejumuisha Idara kadhaa zilimo ndani ya wizara ya nchi, Ofisi ya rais, Katiba, Sheria, Utumishi, Umma na utawala bora pia kilitumika kwa ajili ya afisa mdhamini huyo kujitambulisha kwa wakuu wa Idara

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.