Na Haji Nassor, Pemba
TAASISI ya Kuwajengea
Uwezo Waandishi wa Habari Zanzibar ‘ZJCBF’ ni asasi ya kiraia ya kitaaluma ya uandishi
na utangazaji wa habari Zanzibar.
Kama zilivyo nyengine, nayo taasisi hii iliyoanzishwa kwa
mujibu wa kifungu cha 20, cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na chini ya sheria
namba 6 ya mwaka 1995, inayoruhusu kuanzishwa kwa asasi za kiraia Zanzibar.
Ni taasisi isiyolenga kupata faida binafsi, na imebuniwa
na wanataaluma na wanamaarifa wa masuala ya uandishi na utangazaji wa habari
visiwani humo .
Taasisi hii ilisajiliwa mapema Julai 13, mwaka 2014 na kupewa
namba ya usajili 2292 na Mrajisi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hivyo kwa sasa Zanzibar kuna jumla ya tasisi 11, za kitaaluma
katika masuala ya uandishi na utangazaji wa habari, ambazo zimesajiliwa kama
asasi za kiraia.
Kwa mfano lipo Baraza la Habari Tanzania MCT- Zanzibar, ipo
pia ‘Zanzibar Editors Forum ‘ZEF’, Chama cha waandishi wa Habari wanawake Tanzania
TAMWA- Zanzibar, Klabu ya waandishi wa Habari Zanzibar ZPC, Klabu ya wanahabari
Pemba, ‘PPC’, Jumuia ya waandishi wa Habari za Maendeleo WAHAMAZA.
Taasisi hii ya Kuwajengea Uwezo waandishi wa habari na
watangazaji wa habari, kama vile imekuja na kitu kipya ambacho, waandishi wa
habari wenyewe kimewafurahisha.
Kwa mujibu wa Mkurungenzi wa ZJCBF, Juma Khamis Juma
aliwathibitishia waandishi hao kwenye mkutano uliofanana kama wa uzinduzi,
uliofanyika mjini Unguja, kwamba watapatiwa vifaa.
Wakati akieleza hayo, waandishi waliohudhuria kwenye hafla
hiyo, walikumbwa na mshangao wa furaha, juu ya malengo ya taasisi hiyo kwao.
Maana mtangaazaji Khadij Kombo Khamis wa ZBC redio Pemba,
alionekana kama aliepatwa na kitetemishi cha kauli, juu ya taasisi hiyo
kuwaahidi kuwapatia vifaa.
“Jamani mimi kama sijafahamu, Mkurugenzi unasema kwamba baada
ya kupewa mafunzo, mnamalengo ya kutupatia na vifaa…?’’,alihoji mtangaazaji huyo.
Mtangaazaji Jazaa Kombo wa kituo cha redio cha Hits fm,
alionekana kukazia nati neno la mtangaazaji mwenzake, kwamba, lazima kwenye
hili ukweli uwepo.
Anasema sio sahihi kwa taasisi hiyo, kupanga mipango na
mikakati madhubuti ya kuwaendeleza wanahabari kivifaa, kisha kuingia mitini.
“Maana zipo taasisi zinazofanana na ZJCBF, huahidi mambo
mazuri kwa makundi husika, kisha kutetereka na ahadi kuwa hewa, sasa na hili
lifanyike kweli’’,alifafanua.
Hapo Mwenyekiti Mtendaji wa taasisi hiyo Rajab Khamis Rajab,
alilazimika kutuliza mizuka ya waandishi na kuwaahidi kuwa wameshajipanga.
Anasema hilo limo kwenye mipango na mikakati yao,
ilikuhakikisha waandishi wa habari Zanzibar, bila ya kujali vyombo wanavyotoka
wanapatiwa vifaa.
Taasisi inakusudia baada ya kuwapatia mafunzo, kuwakata kiu
ya kuwapatia vitendea kazi kama vile vinasa sauti, kamera na hata kompyuta.
Wakati akifafanua hilo, mwandishi Salum Vuia Issa wa Idara ya
Habari Maelezo, yeye alitaka atolewe tena hofu juu ya taasisi hiyo kuwapatia
vifaa waandishi.
Vuia haamini sana kwenye nafsi yake, kutokana na Zanzibar
kuanzishwa kwa jumuia kadhaa, zikiwa na katiba zenye malengo mazuri, kisha
wakati wa utekelezaji mambo kwenda ndivyo sivyo.
“Mimi kwanza napongeza hatua ya kujipanga kutupatia vifaa,
lakini lazima ukweli uwepo katika hili, ili kuepusha ahadi hewa kama
wanavyofanya wengine’’,alitahadharisha.
Punde Mkurugenzi Mtendaji wa ZJCBF Juma Khamis Juma,
alisimama wima, akawataka waandishi wawaamini na kuwapa msaada wa ushirikiano,
ili taasisi hiyo ipate mafanikio.
“Hii ni taasisi nyengine na ya kupigiwa mfano, ni tofauti na
hizo nyangine, sasa kama tukishirikiana basi malengo ya taasisi yenu
yatafikiwa’’,alifafanua.
Alisisitiza kila kitu kina simama kikiwa na miguu, na kwamba
kwa taasisi yao, miguu yake ni wanachama ambao ni waandishi wa habari,
watangaazaji na hata wamiliki wa mitandao ya kijamii.
Awali taasisi hii inakusudia kuwajengea uwezo waandishi wa habari,
kwa njia ya mafunzo kwa kujumuisha midia chapishi (magazeti na vitabu), midia-tangazi
(redio na runinga) na midia-mtandao (kurasa za tovuti na blogu).
Hili la kuwawezesha waandishi wa habari kwenye taasisi hii,
limeshatajwa litakuwa la kwanza, kisha ndio wakabidhiwe vifaa kwa ajili ya
kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Wapo waandishi wa habari na watangazaji Zanzibar, ambao
wameonekana kusubiri kwa hamu matunda ya taasisi hiyo, na hasa suala la
kusaidiwa vifaa.
Maana mwandishi na mtangaazaji wa redio Jamii Micheweni Pemba
Time Khamis Mwinyi, anaona kukosekana kwa vitendea kazi, wakati mwengine
hurejesha nyuma kazi zao.
Anasema kwenye redio yao mashine za vinasa sauti na komputa
huwa ni shida unapohitaji kwa ajili ya kufanyia kazi, sasa anaamini ZJCBF kama
ikiwapatia watakuwa imara.
Kubwa aliuukumbusha uongozi wa taasisi hiyo, wakati wa
ugawaji, wasije wakasauiliwa waandishi walioko kisiwa cha Pemba, na kuishia
Unguja pekee.
Kauli kama hiyo, ilielezwa na mtangaazaji Said Suleiman wa
redio Adhana fm, akisema hasa ukosefu wa vitendea kazi ndio changamoto
inayokabili, sasa lazima usawa uwepo.
“Mimi naona mafunzo huwa tunapata kila baada ya muda, lakini
suala la vifaa ndio shida kubwa kwetu, sasa taasisi kama imeshajipanga na hilo
twaikaribisha’’,alifafanua.
Mwandishi mkongwe Mussa Haji Foum anaeandikia shirika la
habari la X-inhua la China, anasema suala la vifaa vya kazi kwa waandishi wa nchi
nyengine sio changamoto tena.
“Sasa na sisi Zanzibar kwa muda mrefu, tunalilia hili la
ukosefu wa vitendea kazi, sasa kama ZJCBF imedhamiria hilo, naipongeza mikono
miwili’’,alifafafanua.
Ameona ni aibu kwa waandishi wa habari kunasa sauti au kupiga
picha kwa kutumia simu za mkononi, jambo ambalo halileti taswira nzuri.
Ndio hilo ambalo Mwenyekiti mtendaji Rajab Khamis Rajab, alidakiza
na kusema taasisi yao haiji kwa mfumo wa zima moto kama baadhi ya wengine
wanavyofikiria.
“Unajua sisi leo ndio kama tunazindua taasisi hii baada ya
kupata ufadhili kupitia Mfuko wa wanawake Tanzania ‘WFT’, lakini tumejipanga na
tumedhamiria kweli’’,alijigamba.
Anachoomba kwa wanahabari wa Zanzibar ni kuiunga mkono
taasisi hiyo na kushiriki katika vikao kadhaa pale watakapowaita, ili kujenga
umoja kwa kweli.
Aliwatoa hofu waandishi hao wa habari kuwa, kutokana na
wafadhili ambao wamashawadokeza juu ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo, hana shaka.
Vifaa kama vinasa sauti, kamera na hata kompyuta aliahidi
kuwa vitapatikana bila ya shaka yoyote, kwa waandishi, wamiliki wa mitando ya
kijamii na watangaazaji.
Wakati taasisi hii ya kuwajengea uwezo waandishi na
watangaazaji habari Zanzibar, ZJCBF ikijiwekea mikakati ya kuwapatia vifaa
waandishi na watangaazaji, imeanza kukabiliwa na changamoto kadhaa.
Moja na kubwa ni ukosfu wa rasilimali watu, ingawa Mkurugenzi
mtendaji Juma Khamis Juma, anasema hilo karibu litakaa sawa kwa kuajiri.
Maana kipindi cha mwaka mmoja ujao kutoka sasa, itaajiri wafanyakazi
watatu, wawili wakiwa wanawake, sambamba na kupanga bajeti yao, ambayo itatatua
baadhi ya changamoto.
Taasisi hii mpya pia, kwa sasa haijakuwa na ofisi yake
rasmi, ingawa inakusudia kupangisha jengo eneo la karibu na Posta mkuu mjini
Zanzibar.
Mei 18, mwaka huu, taasisi hiii baada ya kukutana na
waandishi wa habari zaidi ya 35 kutoka kisiwa cha Unguja na Pemba, kwenye
ukumbi wa Umoja wa watu wenye ulemavu Unguja, imewahakikishia itakuwa bega kwa
bega.
Ndio maana kwa kuanzia, tayari idadi hiyo ya waandishi
wa habari na watangaazaji, wameshapewa elimu ya namna ya kuandika au
kutengeneza vipindi juu ya wanawake.
Uongozi wa ZJCBF umetamka kuwa, sasa kazi ya
kuwakomboa wanahabari, wamiliki wa mitandao na watangaazaji Zanzibar imefika, na
kwao ni kuhakikisha wanaungwa mkono.
No comments:
Post a Comment