Habari za Punde

SMT itaendelea kuiimarisha Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.Suzan Alphonce Kolimba wakati alipofika Ikulu Mjini Unguja leo,[Picha na Ikulu.] 12/10/2016.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na mgeni wake  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.Suzan Alphonce Kolimba wakati alipofika Ikulu Mjini Unguja leo,[Picha na Ikulu.] 12/10/2016.





STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                          12.10.2016
---
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuiimarisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mashirikiano ya pande zote mbili za Muungano ili iendelee kuleta manufaa na kuzidi kuitangaza vyema Tanzania Kitaifa na Kimataifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Susan Alphonce Kolimba aliyefika Ikulu Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweza kujijengea sifa kubwa katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na hata nje na ndani ya Bara la Afrika hivyo, kuimarika kwa Wizara hiyo kutaongeza kasi ya kutekeleza majukumu yake hayo.

Dk. Shein alisema kuwa mashiriakino ya pamoja ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yameweza kuleta mafanikio ndani ya Wizara hiyo, hivyo kuna kila sababu ya kuimarishwa zaidi ili malengo yaliyokusudiwa katika Wizara hiyo yaweze kufikiwa.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa kazi nzuri inaoendelea  kuifanya katika kuhakikisha mafanikio zaidi yanaendelea kupatikana.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliupongeza uwamuzi mzuri wa Naibu Waziri huyo wa kufanya ziara katika Ofisi zake zilizopo hapa Zanzibar kwani atapata fursa nzuri ya kukaa na viongozi pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo na kuzungumza nao masuala mbali mbali ya kazi zao huku akimsisitiza kuwa ziara hizo ziwe endelevu.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alizipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ikiwa ni pamoja na kuendelea kuithamini  Zanzibar na kuishirikisha kikamilifu kwa kutambua umuhimu wake ndani ya Jumuiya hiyo huku akirejea pongezi zake kwa Bunge la Jumuiya hiyo kwa kuja kufanya mkutano wake unaoendelea hapa Zanzibar.

Dk. Shein alimuhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wake katika Jumuiya hiyo ili kuhakikisha kuwa inapata manufaa katika kufikia lengo lililokusudiwa.

Vile Vile, Dk. Shein aliitumia fursa hiyo kumueleza Naibu Waziri huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wake katika kuhakikisha Wizara hiyo inaimarika zaidi ili iweze kuendelea kuwa na sura ya Muungano.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Susan Alphonce Kolimba alimuelezea Dk. Shein shughuli zinazofanywa na Wizara hiyo pamoja na kueleza kazi zinazofanywa na Wizara hiyo ndani ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki hivi sasa.

Dk. Kolimba alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa kuendelea kutoa miongozo na ushauri mzuri ambao umekuwa chachu katika kuendeleza Wizara hiyo na kumpongeza kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa hapo jana katika  Mkutano wa Pili wa Kikao cha Tano cha Bunge la Tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki..

Aidha, Dk. Kolimba alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kutoa fursa sawa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza mashirikiano yanaimarishwa katika kuiongoza Wizara inayoshughulikia Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Pamoja na hayo, Dk. Kolimba alipongeza juhudi za makususdi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein katika kuwaletea maendeleo wananchi wake wote.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.